KINDI-MOSHI.
WIZARA ya Kilimo imesema iko katika hatua za mwisho za kufanya maboresho yatakayowezesha kuanzishwa kwa Wakala wa Ugani, chombo kitakachokuwa na jukumu la kuhakikisha wakulima wanapata elimu stahiki kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Dk. Yasinta Nzogela, wakati wa hafla ya ugawaji wa miche bora ya ruzuku ya parachichi iliyofanyika katika eneo la KNCU, Kijiji cha Kindi, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Dk. Nzogela alisema kuanzishwa kwa wakala huyo kutaleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za ugani, akieleza kuwa kwa sasa maafisa ugani wako chini ya halmashauri hali inayochangia kupungua kwa ufanisi wa huduma hizo.
“Tunataka kuleta mageuzi makubwa kwa kuanzisha wakala wa ugani ambaye atasimamia moja kwa moja huduma hizi. Sera tayari imepitishwa na tuko katika hatua za mwisho, ifikapo Julai mwaka huu tutakuwa na chombo maalum kinachosimamia ugani,” alisema.
Alifafanua kuwa wakala huyo atahakikisha wakulima wanapatiwa elimu sahihi pamoja na vitendea kazi kwa maafisa ugani, zikiwemo pikipiki na vifaa vingine vitakavyowawezesha kuwafikia wakulima mashambani na kuwapa ushauri wa kitaalamu kuhusu kilimo bora.
Aidha, alisema serikali imejipanga kuhakikisha maafisa ugani wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia, kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Katika hatua nyingine, Dk. Nzogela alisema serikali imeanzisha mfumo rasmi wa uzalishaji unaoanzia shambani hadi sokoni, utakaowezesha usajili wa wakulima na kurasimisha shughuli za kilimo, hatua itakayosaidia kuongeza tija na upatikanaji wa masoko yenye uhakika.
“Lengo ni kuhakikisha mkulima anapata haki yake, mnunuzi anapata haki yake, na serikali inakusanya mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za jamii kama barabara, vituo vya afya na shule,” alisema.
Alibainisha kuwa kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakikosa tija kutokana na kutofuata kanuni bora za uzalishaji pamoja na changamoto za masoko, hali inayowakatisha tamaa baadhi yao kuendelea na kilimo.
Dk. Nzogela aliwataka wakulima wa Wilaya ya Moshi kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na serikali, kuzingatia kanuni bora za kilimo na kusimamia vizuri miche waliyopewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nafaka na mazao mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, huku akiwashukuru wabunge wa majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini kwa kusaidia upatikanaji wa fursa hizo kwa wananchi.
Alisema COPRA imetoa mafunzo kwa vijana takribani 100 kwa ajili ya kuwasajili wakulima wote watakaopatiwa miche ya parachichi, hatua itakayosaidia kurasimisha sekta hiyo.
Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, aliwahimiza wananchi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuotesha miche ya parachichi na kahawa ili kuongeza kipato cha familia.
Naye Mbunge wa Vunjo, Enock Zadock Koola, aliishukuru Wizara ya Kilimo kupitia COPRA kwa kugharamia miche hiyo, akieleza kuwa mahitaji ni makubwa na kuomba iongezwe zaidi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.


















