WABUNGE VUNJO, MOSHI VIJIJINI WAPONGEZWA KWA KULETA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WANANCHI


Mbunge Jimbo la Moshi Vijijini Mhe. Morris Makoi na Mbunge wa Jimbo la Vunjo Mhe. Enock Zadock Koola 

KILEMA KUSINI.

WABUNGE wa Majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini , wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamepongezwa kwa juhudi zao za kuwaletea maendeleo wananchi ndani ya kipindi kifupi tangu walipochaguliwa kuingia bungeni.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kilema Kusini, jimbo la Vunjo, katika hafla ya ugawaji wa miche ya parachichi.

Mlola alisema kuwa Mbunge Enock Koola wa Vunjo na Morris Makoi wa Moshi Vijijini wameonesha dhamira ya dhati katika kuwatumikia wananchi kwa kuwatafutia fursa za kiuchumi, licha ya kuwa ni mapema kutathmini utendaji wao wa kibunge.

Alieleza kuwa viongozi hao wameanza vyema kwa kupambania maendeleo ya wananchi wao, hususan katika sekta ya kilimo, jambo linaloleta matumaini ya kupunguza umaskini na kuinua uchumi wa jamii.

Aidha, Mlola alisisitiza umuhimu wa wakulima kusimamia vizuri zao la parachichi, akibainisha kuwa lina fursa kubwa kiuchumi endapo kanuni bora za kilimo zitazingatiwa kuanzia upandaji hadi uvunaji na uhifadhi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Vunjo, Enock Koola, amewahimiza wananchi kuchangamkia kilimo cha parachichi, akisema ni zao lenye uwezo wa kuleta tija kubwa ndani ya muda mfupi.

Alisema kuwa serikali kupitia COPRA imetoa miche 1,000 ya parachichi kwa wakulima wa majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini kwa gharama ya shilingi milioni 400, ikiwa ni jitihada za kukuza sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi.

"Naishukuru sana Wizara ya Kilimo kupitia COPRA kwa kutoa miche bora ya parachichi kwa ruzuku, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima."alisema.

Koola pia aliomba kuanzishwa kwa vitalu vya miche ya parachichi katika jimbo hilo ili kurahisisha upatikanaji wake na kutoa ajira kwa vijana na wanawake, badala ya kuagiza kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Naye Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, aliwataka wananchi watakaonufaika na miche hiyo kuitunza vizuri ili iweze kuleta tija na kuboresha maisha yao.

Awali, Diwani wa Kata ya Kilema Kusini, Ovin Maliti, aliwapongeza wabunge hao kwa maono yao ya maendeleo yanayolenga kuinua uchumi wa wananchi.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.