Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga Mwl. Ibrahim Mnzava, akikabidhi bomba za maji kwa niaba ya Mbunge, kwa mkuu wa shule ya sekondari Toroha.
TOROHA-MWANGA.
WANAFUNZI wa walimu wa shule ya sekondari Toroha iliyoko Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wataondokana na adha ya kutembelea umbali mrefu kutafuta maji baada ya Mbunge wa Jimbo la Mwanga Dk. Ngwaru Maghembe kukabidhi bomba zitakazowezesha upatikanaji wa maji shuleni hapo.
Akikabidhi bomba hizo kwa niaba ya Dk. Maghembe, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga Ibrahim Mnzava, amesema mbunge ametekeleza ahadi hiyo aliyoitoa kwa uongozi wa shule hiyo baada ya uongozi huo kuwasilisha changamoto ya upatikanaji wa maji shuleni hapo.
"Alitoa Ahadi hii wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, ambapo ameleta rola sita zenye urefu wa mita 900 ambazo zitawezesha upatikanaji wa maji hapa shuleni”, alisema Mnzava.
Mkuu wa shule ya sekondari Toroha, Anthony Mziray, alimshukuru Mbunge Maghembe kwa kutimiza ahadi yake hiyo jambo ambalo alisema ni mchango mkubwa kwa shule hiyo kuliko inavyoweza kufikirika.
“Changamoto kubwa katika shule yetu hii kwa miaka mingi ni upatikanaji wa maji; wanafunzi wanalazimika kukatisha vipindi vya masomo ili kwenda kutafuta maji umbali wa kilometa tatu kutoka shuleni hapa”, alisema.
Aliongeza, "Changamoto hii ilinatokana na shule kukosa miundombinu ambayo inawezesha kufikisha maji shuleni hapa kutoka kwenye vyanzo vya maji mbalimbali; bomba hizi ni ukombozi mkubwa kwetu”.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa shuel hiyo, Giftlulu Munuo na Maala Minja, walimshukuru Mbunge kwa kutatua changamoto hiyo ambayo walisema itawaondolea adha kubwa iliyokuwa ikiwanyima kuzingatia masomo yao ipasavyo.
“Huwa hatupati maji ya kutosha kufanya shughuli zetu za kawaida ikiwemo kupikia chakula, kuogea, kufulia nguo na hata kufanya usafi wa madarasa na mabweni yetu; tunateseka sana”, walisema.
Nae Maala Minja alisema mchango huo ni muhimu si kwa wanafunzi tu bali pia kwa walimu ambao alisema walikuwa wanakereka kukatiza vipindi vya masomo ili wanafunzi wakatafute maji.
Awali, Katibu wa CCM wilaya hiyo Mwadawa amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo, ambayo imetumia gharama nyingi kupatikana.
"Pesa ya mfuko wa jimbo ni ndogo sana, haiwezi kukidhi changamoto zote za kata 20, vijiji na vitongoji, hivyo Mbunge hulazimika kutoa posho yake kwa ajili ya kusaidia baadhi ya changamoto zilizoko katika jimbo lake; njia ya kumuunga mkono ni kuhakikisha miundombinu hii inakuwa salama”, alisema.
Katibu wa Mbunge Jeremiah Boniphace Mziray, alisema mchano huo ni sehemu ya ahadi ambazo Mbunge huyo aliahidi kwenye kata za Jimbo hilo.
"Tunachohitaji kutoka kwenu wananchi ni kumpa ushirikiano Mbunge; tayari ameshatoa michango mbalimbali kwenye shule ya msingi Kalamba, Kwakoa, shule ya msingi Mkongea na pia amepeleka tofali 2, 000 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya inayojengwa Kwakihindi, bomba za maji Kivisini, ambapo fedha hizo ni kutoka kwenye mfuko wake," alisema.
Kwa upande wake Mhandisi wa maji Wilaya ya Mwanga (RUWASA) Christine Kessy, alimshukuru Mbunge kwa juhudi zake za kusaidiana na serikali katika kutatua baadhi ya changamoto zilizoko ndani ya wilaya yake ikiwemo suala la maji.
“Tunaimani bomba hizi ambazo amezikabidhi leo katika shule ya sekondari Toroha zitatua changamoto iliyokuwepo ya maji”, alisema Injinia Kessy.
Aidha alisema eneo la Kata ya Toroha ni eneo ambalo linachangamoto kubwa sana ya maji, kutokana na miundombinu yake ni ile ya zamani kuchakaa na ambayo alisema inahitaji kubadilishwa na changamoto nyingine inatokana na tembo kukata bomba kwa ajili ya kutafuta maji.
"RUWASA tunaendelea kuikarabati miundombinu hiyo kadri pesa zinapopatikana kwani ukanda wote wa Tambarare ya Mashariki, bado changamoto ya maji ni kubwa”, alisema.













