KILIMANJARO YAPOKEA SH BILIONI 112.63 KATIKA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA

MOSHI-KILIMANJARO.

MKOA wa Kilimanjaro umepokea jumla ya shilingi bilioni 112.63 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya siku 100 za utekelezaji wa ahadi za Samia Suluhu Hassan, kufuatia kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Kilimanjaro, Ibrahim Urio, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Moshi kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho cha siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema fedha hizo zimeelekezwa katika miradi ya kimkakati, huduma za kijamii pamoja na ajira, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Rais Samia wakati wa kampeni zake mkoani humo.

Katika sekta ya miundombinu, shilingi bilioni 19.7 zimetolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya Ngangamfumuni, huku shilingi bilioni 3.8 zikielekezwa katika ujenzi wa stendi ya mabasi Wilaya ya Mwanga.

Aidha, shilingi bilioni 11.6 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa la Kwasadala, linalotarajiwa kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza mapato kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Katika kuimarisha huduma ya umeme vijijini, mkoa umepokea shilingi bilioni 33.3 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji 186 vilivyokuwa bado havijafikiwa na huduma hiyo.

Urio alieleza kuwa Mkoa wa Kilimanjaro una tarafa 30, mitaa 60, kata 169 na vijiji 159 ambavyo tayari vilishafikiwa na umeme, huku vitongoji 186 kati ya 2,260 vikiwa havijapatiwa huduma hiyo kabla ya fedha hizo kutolewa.

“Lengo ni kuhakikisha wananchi wote wa Kilimanjaro wanapata huduma ya umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Urio.

Katika sekta ya afya, mkoa umeendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote katika halmashauri zote, kupitia mpango wa TASAF, makundi maalumu 41,709 yametambuliwa katika kata na mitaa mbalimbali, na zoezi la uandikishaji linaendelea ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa urahisi.

Aidha, mkoa umepokea watumishi wapya 1,914 katika sekta mbalimbali, ambapo 273 ni wa sekta ya afya, 372 wa elimu na 1,269 ni wa kada nyingine, hatua hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi.

Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hiyo ndani ya siku 100 unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.