Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rau River Michael Massawe wa pili kushoto, akionyesha Mto Rau ulioacha njia yake ya asili na kufuata makazi ya watu, mashamba
MOSHI-KILIMANJARO.
TIMU ya Wataalamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) imeanza tathmini ya awali kwa lengo la kuanza zoezi la kuondoa tope katika mito ya Rau na Ghona, kufuatia maagizo yaliyotolewa na Wqziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro.
Maagizo hayo yalitolewa baada ya Waziri Mkuu kupokea kero ya mafuriko kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, kuhusu madhara yanayosababishwa na mito hiyo kujaa tope na kuhama njia zake za asili.
Akizungumza katika eneo la Kahe Magharibi Wilayani Moshi, Mhandisi wa PBWB, Omary Gumbo, alisema timu hiyo ipo katika hatua ya pili ya tathmini baada ya kukamilisha awamu ya kwanza katika Kata ya Kahe Mashariki.
Alisema Wataalamu hao wamefika Kahe Magharibi kwa kushirikiana na viongozi wa kata na serikali za vijiji kufanya tathmini ya kina ya maeneo yanayokumbwa na mafuriko kila msimu wa mvua za masika.
“Katika ziara yake Jimbo la Vunjo, Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa Bodi ya Maji Bonde la Pangani kuhakikisha changamoto hii inapatiwa ufumbuzi, sisi kama Wataalamu tumeanza kutekeleza maelekezo hayo kwa kufanya tathmini ya awali ili kubaini hatua za kuchukua,” alisema Mhanndisi Gumbo.
Kwa mujibu wa Mhandisi huyo, tathmini ya awali imebaini kuwa mito ya Rau na Ghona imeacha njia zake za asili kutokana na kujaa kwa mchanga na tope linalochangiwa na shughuli za kibinadamu.
Alifafanua kuwa kilimo kinachofanyika ndani ya mita 60 za hifadhi ya mto ni miongoni mwa sababu kuu za kuongezeka kwa tope, hali inayosababisha maji kushindwa kupita katika mkondo wake wa kawaida na badala yake kusambaa katika makazi na mashamba ya wananchi pindi mvua zinaponyesha.
“Tumekuja kubaini maeneo ya kuanza nayo ili kupunguza adha ya mafuriko ambayo imekuwa ikiathiri wakazi wa maeneo haya ya tambarare kila mwaka,” aliongeza.
Naye Mhandisi wa Maji Juu ya Ardhi utoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), Subira Rais, alisema tayari tathmini ya awali imefanyika katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kwamba maandalizi ya kuanza zoezi la udabuaji wa kuondoa tope yanaendelea.
Alisema lengo ni kuhakikisha kazi hiyo inaanza mapema kabla ya kuanza kwa mvua za masika ili kupunguza madhara yanayojirudia kila mwaka.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kahe Magharibi, Abduly Msangi, alisema vijiji vinne vya Kisangesangeni, Miwaleni, Ngasini na Mwangaria ndivyo vinavyoathirika zaidi na mafuriko hayo.
“Tunamshukuru Waziri Mkuu kwa kusikiliza kilio chetu na kutoa maelekezo ya haraka kwa Wataalamu wa Bodi ya Pangani kuja kushughulikia tatizo hili ambalo limekuwa likijirudia kila mwaka,” alisema Msangi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Rau River, Anthony Mushi, alisema Kata ya Kahe Magharibi imekuwa ikikumbwa na mafuriko makubwa kutokana na mto huo kuhama mkondo wake, hali inayosababisha hasara kwa wananchi.
Aidha, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rau Kati, Michael Massawe, alisema changamoto ya Mto Rau imekuwa ikiwasababishia wananchi madhara makubwa baada ya maji kuacha njia zake za asili na kuelekea kwenye makazi ya watu.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha wananchi kushindwa kulima mazao yao huku baadhi ya nyumba zikisombwa na maji wakati wa mvua kubwa.
“Tunashukuru serikali kwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto hii, tunaamini zoezi la kuondoa tope litarejesha mto katika mkondo wake wa asili na kuondoa adha hii,” alisema Massawe.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo, akiwemo Clement Msaki na Peter Kimbori, walisema mafuriko hayo yamekuwa yakiathiri moja kwa moja mashamba yao ambayo ndiyo tegemeo kuu la kipato na chakula kwa familia zao.
Zoezi la kuondoa tope katika mito ya Rau na Ghona linatarajiwa kuwa suluhisho la kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za mafuriko katika Kata za Kahe Mashariki na Kahe Magharibi, huku wananchi wakihimizwa kuzingatia sheria za hifadhi ya mazingira ili kudhibiti urejeaji wa tatizo hilo.













