DK. NGWARU MAGHEMBE, AHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

KOLOMENI-MWANGA.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ngwaru Maghembe, amewataka wananchi wa Jimbo la Mwanga kuhamasika kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira.

Dk. Ngwaru, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, alitoa wito huo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kilomeni, akiwa katika ziara ya kusikiliza na kupokea kero za wananchi kwenye kata mbalimbali za jimbo hilo.

Alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa, pamoja na kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji holela wa miti.

“Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanalenga kulinda afya za watumiaji, lakini pia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa,” alisema Dk. Ngwaru.

Aliongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia.

Alieleza kuwa Agosti 2024, Rais Samia Suluhu Hassan, alizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo, huku hatua za awali zikilenga kufikia asilimia 89.

Dk. Ngwaru aliwataka wananchi kutumia fursa zilizopo kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhamia katika matumizi ya nishati safi, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Aidha, aliiomba Wizara ya Nishati kuongeza kasi ya upanuzi wa mtandao wa usambazaji wa mitungi ya gesi ili huduma hiyo iwafikie wananchi wa vijijini kwa urahisi zaidi.

Baadhi ya wakazi wa Kilomeni walieleza changamoto ya upatikanaji wa mitungi ya gesi, wakisema hulazimika kusafiri umbali mrefu hadi Mwanga Mjini kwa gharama kubwa. Walimuomba Naibu Waziri kusaidia kuvutia wasambazaji wa gesi kufikisha huduma hiyo katika maeneo ya vijijini.

“Serikali inatuhamasisha kutumia nishati safi ya kupikia, lakini huku kwetu mtungi wa gesi tunalazimika kuufuata Mwanga Mjini ambako ni mbali na gharama ni kubwa. Tunaomba huduma hiyo itufikie huku vijijini,” alisema mmoja wa wakazi hao.

Mbali na Kilomeni, Dk. Ngwaru yupo katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni, ambapo tayari ametembelea kata za Kileo, Lang’ata, Toroha, Kwakoa, Ngujini, Kighare, Chomvu, Kigonigoni, Jipendea, Kivisini, Lembeni na Kirya.

Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 90 ya kaya nchini Tanzania bado hutegemea nishati chafu kama kuni, mkaa na mabaki ya kinyesi cha wanyama kwa shughuli za kupikia, hali inayochangia ongezeko la magonjwa yanayotokana na moshi pamoja na uharibifu wa mazingira.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.