MLINZI WA ZAHANATI YA KILOMENI ADAI MALIPO YA SH MILIONI 4.4, AWASILISHA KILIO CHAKE KWA DK.NGWARU.

KILOMENI-MWANGA.

MLINZI wa Zahanati ya Kilomeni, Kasim Ramadhan Baghashe, amewasilisha malalamiko yake kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ngwaru Maghembe, akidai kutolipwa mshahara wake wa jumla ya Shilingi milioni 4,430,000 kwa kipindi cha miaka saba.

Kasim alitoa malalamiko hayo mbele ya Dk. Ngwaru, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kupokea kero za wananchi katika kata mbalimbali za jimbo hilo.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, mlinzi huyo alidai kuwa hajalipwa mshahara tangu alipoanza kazi mwaka 2018 hadi mwaka 2025.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano, alipaswa kulipwa Shilingi 60,000 kwa mwezi, lakini amekuwa akizungushwa kila anapofuatilia malipo yake.

“Ni miaka saba sasa sijalipwa, kila nikifuatilia naambiwa nivumilie, nitalipwa. Nimekuwa nikikesha kwenye baridi nikilinda mali na vifaa vya zahanati, lakini sina malipo,” alilalamika Kasim.

Alisema kiasi anachodai ni mkusanyiko wa mishahara ya miezi yote tangu aanze kazi hiyo, na kumwomba Naibu Waziri kuingilia kati ili aweze kulipwa haki yake.

Akijibu suala hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilomeni, Gift Cosmas Kinyekile, alisema alihamishiwa katika kata hiyo mwaka 2025 na kukuta deni hilo likiwa tayari lipo.

Alieleza kuwa tangu alipowasili, ameanza kushughulikia suala hilo na tayari amemlipa stahiki zake za miezi ya Januari na Februari mwaka huu.

“Nilipofika hapa nililikuta deni hili, nimeanza kulishughulikia na tayari nimemlipa mshahara wa mwezi wa kwanza na wa pili wa mwaka huu,” alisema Kinyekile.

Kwa upande wake, Dk. Ngwaru alitoa maelekezo kwa viongozi wa kata kuhakikisha kuwa mlinzi huyo analipwa fedha zake zote anazodaiwa kwa mujibu wa taratibu, ili kumaliza changamoto hiyo kwa haki na haraka.

Ziara ya Dk. Ngwaru katika Kata ya Kilomeni ni sehemu ya ratiba yake ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Jimbo la Mwanga kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.