DIWANI WA KATA YA KIUSA KHALID SHEKOLOA, ALETA TABASAMU KWA WENYE MAHITAJI KUPITIA MSAADA WA NGUO, VIATU NA VYANDARUA

MAGU-MWANZA.

KATIKA hali ya simanzi na majonzi yanayogusa mioyo ya wengi, watu wenye mahitaji katika Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, wamekuwa wakipitia changamoto nzito za maisha kila uchao.

Wengi wao wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu, wakikosa mavazi ya staha, viatu vya kujikinga na baridi pamoja na mbu hatari, hali inayowaweka katika hatari ya magonjwa na mateso ya kila siku.

Ni simulizi za huzuni zinazoonyesha namna ambavyo baadhi ya familia zimekuwa zikilala sakafuni bila chandarua, watoto wakitembea peku na wazee wakivumilia baridi kali bila nguo za kuwakinga.

Hata hivyo, mwanga wa matumaini ulionekana pale Diwani wa Kata ya Kiusa, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Khalid Shekoloa, alipoamua kugusa maisha yao kwa vitendo.

Kwa moyo wa huruma na upendo wa dhati, alitoa msaada wa nguo, viatu na vyandarua kwa watu wenye mahitaji ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwajali na kusimama nao katika kipindi hicho kigumu.

Hatua hiyo haikuwa tu msaada wa vifaa, bali ilikuwa faraja na ishara ya kuwa hawajasahaulika, wakati wa ugawaji wa msaada huo, machozi ya furaha yalionekana kwa baadhi ya wanufaika.

Baadhi ya wazee walionekana wakitetemeka kwa hisia, wakishika nguo mikononi mwao kana kwamba wamepokea zawadi ya thamani isiyo na kifani, watoto waliovaa viatu vipya kwa mara ya kwanza walitabasamu kwa aibu, huku wazazi wao wakishukuru kimoyomoyo kwa kuona angalau siku hiyo imeleta nafuu katika maisha yao.

Akizungumza diwani huyo alieleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha jamii, inaishi kwa mshikamano na upendo, na kwamba wenye uwezo wanapaswa kuwakumbuka wasiojiweza.

Alisisitiza kuwa msaada huo ni mwanzo tu wa jitihada endelevu za kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupunguza makali ya maisha kwa makundi maalum.

Miongoni mwa maneno ya shukrani kutoka kwa wanufaika ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema kwa sauti ya unyenyekevu: “Tulikuwa tunaishi kwa tabu sana, watoto wangu walilala bila chandarua na kuumwa na mbu kila usiku, leo hii tumepata faraja. 

"Mwenyezi Mungu amlinde sana huyu Diwani kwa kutona sisi wenye uhitaji," alisema mmoja wa wanufaika.

Hata hivyo kauli yake iliungwa mkono na wengine waliokiri kuwa msaada huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao.

"Sikuwahi kufikiria kama kuna siku nitapewa msaada wa nguo na viatu bila malipo, kitendo hiki kimetugusa sana, kwanza hatukuwahi kupata misaada kama hii, tunaomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema na ambariki kwa moyo wake wa huruma.” 

Shukrani hizi ziliambatana na sala na baraka nyingi kutoka kwa jamii nzima, kwa ujumla, tukio hilo limeacha alama ya upendo na mshikamano katika Kata ya Nyanguge, ukumbusho kuwa katika nyakati za majaribu, bado wapo wanaochagua kuwa sauti na msaada kwa wasiojiweza.

Hatua ya Diwani Khalid Shekoloa imeleta tumaini jipya, na kuamsha ari ya jamii kuendelea kushirikiana, kujali na kuthaminiana kama ndugu.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.