SIHA-KILIMANJARO.
WAGONJWA wa Kifua Kikuu (TB) wametakiwa kuzingatia kikamilifu ratiba ya matumizi ya dawa na kukamilisha dozi wanazoandikiwa na wataalamu wa afya ili kuepuka kujenga usugu wa dawa unaoweza kusababisha matibabu kuwa magumu na kuchukua muda mrefu.
Rai hiyoimetolewa Novemba 14,2026 na Afisa Muuguzi Msaidizi wa Kitengo cha Kifua Kikuu Sugu kutoka Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI), Jestina Anangisye, wakati wa bonanza la michezo lililoandaliwa kwa ajili ya kuwaimarisha kiafya wagonjwa hao.
Alisema matibabu ya TB ya kawaida huchukua kipindi cha miezi sita, hivyo wagonjwa wanapaswa kuhakikisha wanameza dawa kila siku na kwa wakati uliopangwa na wataalamu ili kupata nafuu na kupona kabisa, huku akieleza kuwa TB inatibika na dawa zake zinapatikana bure katika vituo vya afya vya Serikali nchini.
"Moja ya changamoto tunazokutana nazo wauguzi tunaohudumia wagonjwa hawa ni baadhi yao kukataa kutumia dawa wanazopewa, kutokana na kukosa imani kuwa wanaweza kupona, hali inayosababisha wengine kuwa wagumu kufuata maelekezo ya matibabu."alisema Anangisye.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa TIDI, Wazoeli Mshana, alisema baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakitumia njia zisizo sahihi, ikiwamo kuficha dawa chini ya ulimi na kujifanya wamezimeza, kisha kuzitema chooni baada ya muuguzi kuondoka.
Mshana aliwataka wagonjwa hao kuwa waaminifu katika matibabu yao kwa kufuata maelekezo ya madaktari na kumeza dawa zote wanazoandikiwa, akisisitiza kuwa kutokamilisha dozi kunaweza kuchangia usugu wa vimelea vya TB dhidi ya dawa na kuongeza ugumu wa matibabu.
Akizungumzia uzoefu wake wa matibabu, Agnes Steven, mkazi wa Mkoa wa Morogoro, alisema hali yake ya afya ilikuwa mbaya kabla ya kuanza matibabu, ambapo alikuwa akishindwa kupumua vizuri kutokana na kubanwa na kifua, lakini baada ya kupatiwa elimu na kufuata ratiba ya dawa, afya yake imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Alisema matumizi sahihi ya dawa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu yamekuwa na mchango mkubwa katika kurejesha afya yake, akieleza kuwa hali aliyokuwa nayo wakati anafikishwa kwa matibabu ni tofauti kabisa na aliyonayo sasa.
Naye Yoel Labia, Joseph Mgaya, Rock Shempemba pamoja na Hassan Kilama, walisema elimu kuhusu umuhimu wa kutumia dawa imewasaidia wagonjwa wengi waliokuwa wakikataa matibabu na kuficha dawa, huku wengine wakizitema chooni, kubadilika na kuanza kufuata maelekezo ya wataalamu, hali iliyowasaidia kurejesha afya zao na kuanza kushiriki katika shughuli za kimwili ikiwamo kukimbia na kucheza michezo.
![]() |


















