MAAFISA UGANI 36 WAPATIWA MAFUNZO YA KUONGEZA UBORA WA KAHAWA

MOSHI-KILIMANJARO.

MAAFISA ugani 36, wakiwemo wakaguzi wa zao la kahawa kutoka mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa mafunzo maalumu yanayolenga kuimarisha ujuzi wao katika uzalishaji na usimamizi wa ubora wa kahawa ili kuwasaidia wakulima kuongeza tija na kupata kahawa yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano wa TARI TaCRI, Dk. Marco Magesa, alisema mafunzo hayo kwa maafisa ugani yamelenga kuwajengewa uwezo kuhusu namna ya kukarabati mashamba ya kahawa yaliyopungua uzalishaji.

Sambamba na mafunzo hayo pia walifundishwa matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu, pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo zinazoweza kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao hilo

Alisema maafisa ugani wana mchango wao katika kuwahudumia wakulima wa kahawa, huku akiwahimiza kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na ushauri wa kitaalamu kwa wakulima wanaohitaji mwongozo kuhusu uzalishaji wa zao hilo.

"Mafunzo hayo yalitolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia kituo chake cha Utafiti wa Kahawa cha TARI TaCRI, katika ukumbi wa TCCCo mjini Moshi, lengo likiwa ni kuwajengewa uwezo kuhusu namna ya kukarabati mashamba ya kahawa yaliyopungua uzalishaji,"alisema Dk. Magesa.

Aidha, maafisa ugani hao walipatiwa elimu kuhusu hatua muhimu za utunzaji wa kahawa baada ya kuvunwa, ikiwemo uchumaji, umenyaji na ukaushaji, ili kuhakikisha kahawa inayozalishwa inakuwa na ubora unaoweza kuongeza ushindani wake katika masoko.

Alisema mafunzo hayo kwa maafisa ugani ni kuwa na uelewa sahihi wa teknolojia na kanuni bora za kilimo cha kahawa ili waweze kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za uzalishaji na kuboresha ubora wa mazao yao.

Mafunzo hayo yalitolewa na TARI TaCRI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa, wakiwemo Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), katika jitihada za kuimarisha ujuzi wa wataalamu wanaowahudumia wakulima na kuchochea maendeleo ya sekta ya kahawa nchini.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.