MOSHI-KILIMANJARO.
DIWANI wa Kata ya Kiusa katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Khalid Shekoloa, amewatunuku zawadi mbalimbali wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliofanya vizuri katika masomo yao, ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha kuendelea kusoma kwa bidii na kufikia malengo yao ya kielimu.
Zawadi hizo zilizojumuisha mabegi ya shule, madaftari, kalamu, soksi na saa za mkononi, zilitolewa Novemba 13, 2026, kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Jamhuri na Muungano pamoja na Shule ya Sekondari Kiusa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi zawadi hizo, Shekoloa alisema utoaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri umekuwa utaratibu wake wa kila muhula, akieleza kuwa lengo ni kutambua juhudi za wanafunzi, kuwapa motisha na kuwahamasisha wengine kuongeza bidii katika masomo.
![]() |
Alisema wanafunzi wa elimu ya awali na shule za msingi, kuanzia darasa la awali hadi la saba, walioshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu walikabidhiwa mabegi, madaftari na kalamu, huku wanafunzi wa sekondari wakipatiwa mabegi, madaftari, soksi pamoja na saa za mkononi.
Shekoloa aliwataka wanafunzi hao kutambua umuhimu wa elimu na kuitumia vizuri fursa waliyoipata ya kusoma, akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi muhimu wa maisha yao na mafanikio yao ya baadaye.
Alisema: “Mpo hapa shuleni kwa sababu maalumu, hivyo kila mmoja wenu ahakikishe anatimiza malengo yake kwa kusoma kwa bidii na kutokuwa mtovu wa nidhamu. Elimu bila nidhamu hakuna mafanikio.”
Aidha, aliwapongeza walimu wa shule zilizopo ndani ya Kata ya Kiusa kwa kujitoa katika kutekeleza majukumu yao ya ufundishaji, akisema juhudi zao zimechangia shule za msingi zilizopo katika kata hiyo kuwa miongoni mwa shule kumi bora, hivyo kuwataka kuendelea kuongeza bidii katika kuboresha kiwango cha elimu.










