WALIMU SHIRIMATUNDA WAOMBA MATRONI, VIFAA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU

MOSHI-KILIMANJARO .

WALIMU wa Shule ya Msingi na Awali Shirimatunda, iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kusaidia upatikanaji wa matroni na vifaa vya kufundishia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, wakiwemo wenye changamoto za kiakili na usonji.

Wamesema upungufu wa matroni unawalazimu walimu kusitisha vipindi vya masomo ili kuwasaidia wanafunzi hao katika mahitaji yao binafsi, ikiwemo kwenda chooni na kufanya usafi, hali inayopunguza muda wa ufundishaji.

Akizungumza wakati wa kupokea misaada iliyotolewa na Umoja wa Wanawake Tanzania, UWT Wilaya ya Moshi Mjini, mwalimu wa shule hiyo, Isaack Mwekwa, amesema uwepo wa matroni ungewawezesha walimu kuzingatia zaidi majukumu yao ya ufundishaji huku wanafunzi wakipata huduma wanazohitaji.

Amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa makoti maalumu ya kujikinga wakati wa kuwahudumia wanafunzi hao, pamoja na vifaa vinavyofaa kwa ufundishaji, ikiwemo trampolini, ambavyo vinaweza kusaidia katika shughuli za kujifunza na mazoezi kulingana na mahitaji yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, amesema katika kuadhimisha Wiki ya UWT, umoja huo hufanya matendo ya huruma kwa kutembelea makundi yenye uhitaji na kushiriki shughuli za kijamii, akieleza kuwa wameguswa kusaidia wanafunzi hao ili kuboresha mazingira yao ya kujifunzia.

Aidha Komba ameishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya kwa watu wenye walemavu ambayo imewawezesha kupata elimu na malezi pindi wanapokuwa ahuleni.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Japhet Msuya na Suzan Mika, wameishukuru UWT Moshi Mjini kwa misaada hiyo na kuwataka wadau wengine kuendelea kushirikiana na shule hiyo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kuwawezesha kupata elimu katika mazingira salama na rafiki.























Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.