MUWSA YAPONGEZWA KUTEKELEZA MAAGIZO YA WAZIRI MKUU

 


MOSHI-KILIMANJARO .

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), imepongezwa kwa kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, pongezi hizo amezitoa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo kutoka kwa Mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe.

Mhandisi Kundo alisema utekelezaji unaofanywa na MUWSA unaonesha juhudi za kuhakikisha wananchi katika maeneo mbalimbali wanapata huduma ya maji, huku akiitaka mamlaka hiyo kuendelea kusimamia miradi hiyo hadi ikamilike na huduma kuwafikia wananchi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji, Mhandisi Limbe alisema katika Kata ya Uru Mashariki tayari MUWSA imepokea mabomba, huku kazi ya ulazaji wa mabomba hayo ikiendelea.

Alisema katika Kata ya Marangu Mashariki, MUWSA imepata mabomba kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa mtandao wa maji wenye urefu wa kilomita 13, ambapo hadi sasa kilomita nane za mabomba zimekwishalazwa na kazi ya uchimbaji wa mitaro inaendelea.

Aidha, Mhandisi Limbe alisema MUWSA imeboresha vyanzo viwili vya maji vinavyozalisha lita 50 kwa sekunde, huku akieleza kuwa kwa siku vyanzo hivyo vinazalisha zaidi ya lita zaidi ya 2,000 za maji.

Kwa upande wa Kata ya Mwika Kaskazini, alisema mabomba tayari yamewasili, huku changamoto iliyokuwepo ikiwa ni kupata kibali cha kuingia ndani ya hifadhi, ambacho tayari kimepatikana na hivyo utekelezaji wa mradi huo utaendelea.

Mhandisi Limbe alisema miradi inayotekelezwa katika Kata za Marangu Mashariki na Uru Mashariki inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, hatua itakayowawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma ya maji.

Naibu Waziri Kundo pia alimpongeza Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa MUWSA, Mhandisi Innocent Lugodisha, kwa usimamizi wa utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha maagizo ya Serikali yanafanyiwa kazi.

“Hongera sana kwa kumsaidia Mkurugenzi katika majukumu haya, mkurugenzi ana majukumu mengi na hawezi kufika kila eneo, lakini katika masuala ya miundombinu inapotekelezwa vizuri, ni sehemu ambayo Mkurugenzi wa Ufundi anapaswa kupongezwa,” alisema Mhandisi Kundo.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.