NAIBU WAZIRI AWAAGIZA PBWB KUWAONDOA WANAOISHI MITA 60 ZA VYANZO VYA MAJI

MOSHI-KILIMANJARO.

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameiagiza Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) kuwaondoa wananchi wote waliojenga au wanaoishi ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji, akisema hatua hiyo inalenga kulinda vyanzo hivyo na usalama wa wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.

Mhandisi Kundo ametoa agizo hilo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati wa kikao chake na watendaji wa sekta ya maji kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).

Amesema wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanapaswa kuondoka, kwa kuwa endapo watakumbwa na madhara yatokanayo na mafuriko wakati wa mvua za El Niño, serikali inaweza kulaumiwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa wananchi.

Amesema utaratibu wa kuweka eneo la mita 60 kutoka vyanzo vya maji haukulenga kulinda vyanzo pekee, bali pia kuwaepusha wananchi na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mafuriko.

“Maagizo yangu kwa Bonde la Pangani ni kwamba hatutakubali kuona mwananchi akiendelea kuishi ndani ya mita 60, nendeni mkawaondoe katika maeneo hayo, madhara yakitokea wqkulaumiwa ni sisi Serikali, na fedha ambazo zingetumika kwenye miradi zitatumika kama fedha za uokoaji kutokana na madhara yatakayojitokeza,” amesema.

Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa PBWB kuhakikisha bodi hiyo inajiandaa kwa kutenga fedha za ununuzi na matengenezo ya vipuli vya mitambo, ili wakati wa mvua za El Niño endapo mitambo itapata hitilafu, vipuli vipatikane kwa haraka na kazi ya kuondoa tope kwenye mito iendelee bila kusimama.

“Heri tukose fedha za kutekeleza miradi mipya kuliko kukosa fedha za kuokoa miundombinu yetu iliyoharibiwa na mvua kutokana na mazingira yanayoweza kusababisha maafa kwa wananchi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amesema sekta ya maji ni moja na kwamba changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta hiyo mkoani Kilimanjaro si za PBWB, MUWSA, RUWASA au mamlaka nyingine moja pekee, bali zinapaswa kushughulikiwa kwa ushirikiano.

Amesema watendaji wa taasisi zote zinazohusika na sekta ya maji wanapaswa kuwa tayari kwenda kusaidiana pale changamoto inapotokea, badala ya kusema kuwa jambo hilo ni jukumu la taasisi fulani.

“Tuendelee kufanya kazi kama timu moja na si kusema kwamba hiyo ni kazi ya watu wa Bonde la Pangani,” amesema.

Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa PBWB, Mhandisi Segule Ally Segule, kujenga mahusiano mazuri na wakandarasi wenye mitambo ya ujenzi, ikiwemo eksaveta na buldoza, ili mitambo hiyo iweze kutumika kwa haraka pale mafuriko yanapotokea na kuhitajika katika shughuli za uokoaji na urejeshaji wa miundombinu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa PBWB, Mhandisi Segule Ally Segule, amesema bodi hiyo tayari imeanza kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, ikiwemo shughuli za kuondoa tope katika Mto Ghona na Mto Rau.

Amesema katika maeneo ya Mkata na Kilindi, PBWB tayari imefanya utafiti na kupeleka mitambo kwa ajili ya kuanza shughuli za kuondoa tope katika mito hiyo.

Amesema katika Mto Ghona, kati ya kilomita 10 zinazohitaji kuondolewa tope, tayari kilomita saba zimefanyiwa kazi, huku katika Mto Rau zikiwa zimefanyiwa kazi kilomita tisa na shughuli hiyo ikiendelea.

Hata hivyo, Mhandisi Segule amesema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni upatikanaji wa fedha za kuendelea na utekelezaji wa shughuli hizo za kuondoa tope na kuboresha miundombinu ya maji.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.