MOSHI-KILIMANJARO.
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewaaga waandishi wa habari mkoani humo wanaoshiriki ziara maalumu ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, akiwataka kutumia ziara hiyo kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Babu ametoa wito huo ofisini kwake mkoani Kilimanjaro, wakati akiwaaga waandishi hao wanaokwenda Mkomazi kwa lengo la kujionea shughuli za uhifadhi pamoja na vivutio mbalimbali vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Amesema ziara hiyo ni fursa muhimu kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira, sambamba na kuhamasisha wananchi kushiriki katika kutunza rasilimali hizo.
Amesema waandishi wanapaswa pia kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, ikiwemo umuhimu wa wananchi kuzingatia taratibu za uhifadhi na kulinda mazingira yanayowazunguka.
“Waandishi wa habari mtumie kalamu zenu kuelimisha jamii kuhusu ulinzi wa wanyamapori na ikolojia, pamoja na namna ya kuepuka migogoro kati ya binadamu na wanyama,” amesema Babu.
Aidha, Babu amesema Kanda ya Kaskazini ina vivutio vingi vya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Arusha National Park, Manyara, Tarangire, Ngorongoro na Serengeti, hivyo Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio hivyo kama sehemu ya kukuza utalii wa ndani.
Katika hatua nyingine, Babu amemshukuru Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa TANAPA, Mkuu wa Hifadhi Kanda pamoja na Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, kwa kukubali ombi la waandishi wa habari kutembelea hifadhi hiyo, akisisitiza kuwa ziara hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi na fursa za utalii nchini.
Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Msafara, Lawrence Lisakeli, amesema ziara hiyo imelenga kuwapa waandishi wa habari fursa ya kujionea kwa vitendo shughuli za uhifadhi, vivutio vya utalii pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.












