IDADI YA WATALII HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI YAONGEZEKA”

"

SAME-KILIMANJARO.

IDADI ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi imeongezeka kutoka watalii Elfu Tatu kabla ya kuanzishwa kwa utalii wa Faru Weusi mwaka 2021, hadi kufikia takribani Watalii Elfu Kumi hadi Septemba mwaka huu

.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Eva Mallya, amesema ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuanzishwa na kutangazwa kwa utalii wa Faru Weusi, ambao umekuwa kivutio kikubwa kwa wageni.

Alisema Faru Mweusi ni miongoni mwa wanyama wanaowavutia watalii wengi kutokana na nafasi kubwa ya kumuona akiwa katika mazingira yake ya asili.

Alisema Hifadhi ya Mkomazi imekuwa ikijinasibu kwa kauli isemayo, “Njoo Hifadhi ya Mkomazi, utakuwa na uhakika wa asilimia 99 kumuona faru,” akieleza kuwa mgeni anaweza kumuona faru huyo kwa karibu na kupata fursa ya kupiga picha.

Alisema mbali na Faru Weusi, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ina vivutio mbalimbali, ikiwemo Mbwa Mwitu ambao pia wako katika hatari ya kutoweka, pamoja na Swala Twiga, Tembo, Simba, Chui, Nyati na Twiga.

Aidha, hifadhi hiyo ina zaidi ya aina 450 za ndege, huku watalii wakipewa fursa ya kufanya utalii wa mchana, usiku, matembezi kwa miguu, kupiga picha na kutembelea maeneo ya makambi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi anayesimamia shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Geofrey Kyando, amesema Swala Twiga ni miongoni mwa vivutio vya kipekee vinavyopatikana katika hifadhi hiyo.

Alisema mnyama huyo ana shingo ndefu inayofanana na Twiga na hula majani katika vichaka vifupi, huku akieleza kuwa watalii wanaweza pia kuwaona mbwa mwitu pamoja na wanyama wengine wanapofanya safari za utalii ndani ya hifadhi.

Baadhi ya waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo akiwemo Jerome Kulwa na Julitha Mushi, walisema ziara hiyo imewapa nafasi ya kujionea kwa vitendo utajiri wa vivutio vilivyopo Mkomazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwataka waandishi wa habari kutumia ziara hiyo kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Katika ziara hiyo Waandishi walitembelea eneo la Mbula, ambako kuna mradi wa Faru Weusi, maeneo ya malazi ya wageni, eneo la Mbwa Mwitu na maeneo mengine ya hifadhi, na hapo ndipo Mkomazi inapoanza kueleweka kwa picha tofauti.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.