TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imezitaka halmashauri nchini kuweka wazi taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, ili kuwawezesha wananchi kuifahamu, kuifuatilia na kutoa taarifa zitakazosaidia kuzuia ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Kaulli hiyo imetollewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Crispin Chalamila, wakati akizindua jengo jipya la Ofisi za Takukuru Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, lililogharimu Shilingi milioni 405.5.
Chalamila alisema ni muhimu wananchi kushirikishwa katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Serikali zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na thamani ya fedha inaonekana.
“Ni azma ya Takukuru kuona miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kiwango cha juu na ubora unaostahili, tunataka kuona fedha zinazopelekwa kwenye miradi zikionekana, lakini pia utekelezaji wake uwe wa uwazi na uwajibikaji,” alisema.
Alisema kila halmashauri inapaswa kuwa na utaratibu wa kutangaza miradi iliyopitishwa, ikiwamo kubandika taarifa zake kwenye mbao za matangazo, ili wananchi waweze kuifahamu na kushiriki katika ufuatiliaji wa utekelezaji wake.
“Wananchi wanapotangaziwa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, wanapata nafasi ya kuifuatilia na kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kuzuia udokozi na ubadhirifu wa fedha, pia wanaweza kutoa mawazo chanya yatakayosaidia miradi kutekelezwa vizuri kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Aidha, Chalamila alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa majengo ya ofisi za Takukuru nchini, akisema hatua hiyo inaipa taasisi hiyo mazingira bora ya kutekeleza majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Alisema katika mwaka wa fedha 2026/27, Takukuru inajenga majengo 12, yakiwamo mawili ya ofisi za mikoa na 10 za wilaya, na kwamba ifikapo Juni 30, 2027, taasisi hiyo itakuwa na jumla ya majengo 93 ya ofisi nchini.
“Serikali imetuwezesha kwa kiasi kikubwa sana na hili kwetu ni deni tunalopaswa kulilipa, hatuna budi kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii zaidi na kwa weledi ili dhamira ya Serikali ya kutokomeza rushwa nchini iweze kufikiwa,” alisema
Kwa upande wake, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Mussa Chaulo, alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza Desemba 2025 na kukamilika Juni 2026
Alisema Wilaya ya Hai ilianzishwa mwaka 2002, huku eneo la ofisi ya Takukuru likipatikana mwaka 2016 na mchakato wa kupata hati ya umiliki wa eneo hilo ukakamilika mwaka 2024, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo hilo Desemba 2025.
Awali, akiwasilisha taarifa kuhusu ujenzi wa ofisi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Milki Makao Makuu ya TAKUKURU Frank Mkilanya, alisema kuwa mradi huo uligharimu zaidi ya shilingi milioni 405, kutokana na bajeti iliyokadiriwa ya zaidi ya shilingi milioni 407 kwa ajili ya kazi hiyo.
"Takwimu zinaonyesha wazi kuwa usimamizi makini wa fedha ulisababisha kuokolewa kwa zaidi ya shilingi milioni 2; pamoja na bakaa hiyo, mradi wenyewe pia umeonyesha thamani halisi ya fedha zilizotumika katika utekelezaji wake," alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Rukia Zuber, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
Alisema jengo hilo ni muhimu kwa wananchi wa Hai kwa kuwa litasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za Takukuru na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo wilayani.







