MOSHI-KILIMANJARO.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro kimewataka madiwani kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ili kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Julius Peter, aliyasema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini, katika kikao chake cha kwanza tangu alipohamishwa kutoka Mkoa wa Njombe na kupewa jukumu la kuongoza chama katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Julius alisema madiwani wanapaswa kufanya ziara katika maeneo ya kata zao na kuzungumza na wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili, huku akisisitiza kuwa ziara hizo zinapaswa kutambuliwa na chama na viongozi wa chama kushirikishwa.
Alisema hatua hiyo itasaidia wananchi kupata fursa ya kueleza kero zao na kupata majibu kwa wakati, badala ya kusubiri viongozi kutoka ngazi za juu wanapofanya ziara katika maeneo yao.
“Unaposikiliza changamoto na kero za wananchi unapunguza maswali ambayo hujitokeza wakati viongozi kutoka ngazi za juu wanapokuja, maswali mengi yanaweza kujibiwa hapa kwa kuwa madiwani wapo karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Aidha, alisema mikutano hiyo ni muhimu kwa kuwawezesha wananchi kufahamu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na kupata fursa ya kueleza changamoto zinazohitaji kushughulikiwa na viongozi wao.
Katika kikao hicho, Julius pia alikutana na Baraza la Wazee wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, ambapo aliwataka viongozi wa chama kuimarisha ushirikiano na viongozi wa serikali ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Pia aliwataka Wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro kufanya ziara katika maeneo yao ili kusikiliza kero za wananchi na kuwaeleza kazi walizozifanya tangu walipochaguliwa kuwa wawakilishi wao bungeni.
“Wabunge ambao tuliwateua kupeperusha bendera ya CCM, nawataka muendelee kuimarisha mshikamano, mahusiano na umoja, kwani umoja ndio unaoleta mafanikio, mnaposhirikiana kwa pamoja mnaweza kuleta maendeleo kwa wananchi, sitarajii kuona mnaendeleza mipasuko,” alisema.
Pia aliwaomba viongozi wa chama na watendaji wa serikali kuendelea kushirikiana katika kipindi chote atakachokuwa akitekeleza majukumu yake mkoani Kilimanjaro, akisisitiza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kuimarisha mahusiano na kuharakisha utatuzi wa changamoto za wananchi.
![]() |
![]() |










