MASAUNI KUONGOZA KUFUNGA SHUGHULI ZA FLORESTA-SAME

SAME-KILIMANJARO.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha shughuli za Floresta Tanzania katika Mkondomaji wa Saseni, Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Oktoba 15, mwaka huu, katika Kata ya Mamba Miamba, viwanja vya Shule ya Sekondari Parane, ambapo inatarajiwa kukutanisha washiriki wapatao 5,000, wakiwemo wanamazingira, vikundi vya VICOBA, wasanii na wadau mbalimbali.

Mkurugenzi wa Floresta Tanzania, Richard Mhina, alisema kuwa lengo la hafla hiyo ni kumshukuru Mungu kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote ambacho taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli zake za uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii katika Mkondomaji wa Saseni.

Mhina alisema kuwa uwepo wa Waziri Masauni katika hafla hiyo utaenda sambamba na hitimisho la shughuli za Floresta Tanzania katika eneo hilo, huku akieleza kuwa utekelezaji wa miradi ya taasisi hiyo umechangia kuboresha maisha ya wananchi pamoja na mazingira katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alisema miradi ya Floresta Tanzania imekuwa na mchango katika juhudi za kupunguza umaskini na kulinda mazingira, huku wananchi wakinufaika na shughuli mbalimbali zilizotekelezwa katika kipindi chote cha mradi.

Hata hivyo, Mhina alisema utekelezaji wa shughuli hizo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo shughuli za kibinadamu kama uchomaji wa misitu, kilimo katika maeneo ya vyanzo vya maji na ukataji miti holela, ambazo kwa kiasi kikubwa zilichangia uharibifu wa mazingira.

Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha athari mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya misimu ya mvua na kuathiri shughuli za kilimo zinazotegemewa na wananchi.

Alieleza kuwa hafla hiyo pia itakuwa fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana na kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.