MOSHI-KILIMANJARO.
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, amepongezwa kwa kuanzisha mifumo ya kidijitali inayolenga kuongeza uwazi, kuboresha usambazaji wa miche bora na kuinua ubora wa kahawa inayozalishwa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCB, Profesa Aurelia Kamuzora, wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Kahawa la mwaka 2026, msimu wa saba, linalofanyika katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha TCCCo jijini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Profesa Kamuzora amesema mifumo hiyo imeleta mabadiliko katika usimamizi wa zao la kahawa, huku akiwataka wakulima kufuata ushauri wa wataalamu ili kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa kahawa.
Amesema mfumo huo unasaidia kuongeza uwazi katika usambazaji wa miche bora kwa wakulima, huku mikoa ya Kagera, Ruvuma na Mbeya ikiwa miongoni mwa maeneo yaliyoanza kuutumia.
Aidha, Profesa Kamuzora ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono matumizi ya mifumo hiyo, akieleza kuwa ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la Taifa la kuzalisha tani 300,000 za kahawa ifikapo mwaka 2030.
Amesema mifumo hiyo pia itasaidia kufuatilia kahawa kuanzia mashambani hadi sokoni na kuongeza ushindani katika soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Hassan Bomboko, amesema uzalishaji wa kahawa nchini umeongezeka kutoka tani 67,000 wakati Rais Samia alipoingia madarakani hadi tani 85,000 kwa sasa.
Bomboko ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amewataka wadau kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji, uchakataji na biashara ya kahawa ili kuongeza ufanisi na thamani ya zao hilo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Denis Mahulu, amesema tamasha hilo la msimu wa saba ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani, yanayofanyika Oktoba Mosi kila mwaka, likilenga kutambua mchango wa wakulima na wajasiriamali pamoja na kuwaunganisha wadau wa sekta hiyo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha mnyororo wa thamani wa kahawa nchini.









