MWENGE WA UHURU KUTEGEMEA MIRADI SABA YA MAENDELEO MANISPAA YA MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO .

MKUU wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili mkoani Kilimanjaro Juni 28, 2026 ukitokea mkoa wa Tanga, ambapo utakimbizwa katika wilaya zote za mkoa huo kabla ya kuhitimisha mbio zake katika Manispaa ya Moshi Julai 2 mwaka huu.

Mnzava alisema baada ya kupokelewa mkoani Kilimanjaro, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya za Same, Mwanga, Rombo na Moshi Vijijini kabla ya kuingia Manispaa ya Moshi, ambapo mapokezi rasmi yatafanyika katika Shule ya Msingi Msaranga.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya ujio wa mwenge huo, alisema utakagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Moshi.

Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Barabara ya Makanya iliyopo Kata ya Majengo, mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lucy Lameck pamoja na jiko la kisasa linalotumia nishati safi, ambalo linatarajiwa kuboresha mazingira ya upishi na kuhifadhi mazingira.

Aidha, alisema Mwenge wa Uhuru utatembelea chanzo cha maji cha Moshi ambapo utakagua mradi wa maji unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi, pamoja na kuzindua mradi wa Kituo cha Lori katika Kata ya Karanga uliojengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe.

"Manispaa ya Moshi imeendelea kutekeleza sera ya uwezeshaji wa makundi maalum kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, hivyo mwenge huo utapata fursa ya kutembelea kikundi cha vijana cha B5 Media kilichopo katika jengo la Kahawa House ili kujionea shughuli za utangazaji na habari zinazofanywa na wanufaika wa mikopo hiyo."alisema.

Aliongeza kuwa dhana ya Mwenge wa Uhuru pia inalenga kuhamasisha uwekezaji na maendeleo ya sekta binafsi, ambapo mwenge huo utatembelea ukumbi mkubwa wa mikutano uliojengwa na kampuni ya Mahina Holding kabla ya kuelekea Uwanja wa Mashujaa kwa shughuli za mkesha wa Mwenge wa Uhuru.

Mnzava amewahimiza wananchi wa Manispaa ya Moshi kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli za mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kutembelea miradi mbalimbali itakayokaguliwa, akisema ujio wa mwenge huo ni fursa ya kuonesha mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana katika manispaa hiyo.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.