MAZOEZI YATAJWA SILAHA MUHIMU YA KUKABILIANA NA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA



MOSHI-KILIMANJARO.

WADAU wa michezo katika Manispaa ya Moshi wameendelea kuhimiza wananchi kushiriki mazoezi ya mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, wakieleza kuwa mazoezi ni njia rahisi na yenye manufaa makubwa katika kuboresha afya na kuongeza tija katika jamii.

Kauli hiyo ilitolewa Juni 20, 2026 na Mratibu wa EFM Jogging Manispaa ya Moshi, Theresia Komba, baada ya kushiriki matembezi ya amani yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya utayari wa mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Julai 2,2026 katika Manispaa ya Moshi.

Komba alisema kuwa wanamichezo na wadau mbalimbali wa mazoezi wamekuwa wakikutana kila Jumamosi kushiriki shughuli za michezo na mazoezi ya viungo kwa lengo la kuimarisha afya zao na kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Alisema kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika mazoezi kutasaidia kupunguza gharama kubwa zinazotumika kutibu magonjwa hayo, hivyo kuwezesha Serikali kuelekeza rasilimali zaidi katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.

Aidha, Komba aliwataka wananchi kuendelea kufanya mazoezi kwa kujumuika katika vilabu vya michezo na vikundi vya jogging, akisisitiza kuwa afya bora hujengwa kupitia mtindo mzuri wa maisha unaojumuisha mazoezi ya mara kwa mara na lishe sahihi.

Pia alitumia fursa hiyo kuhimiza jamii kuendelea kudumisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa uliowekwa na waasisi wa Taifa, akieleza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi wa maendeleo ya michezo na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Matembezi hayo yaliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, yakishirikisha Kamati ya Usalama ya Wilaya, viongozi wa Manispaa ya Moshi wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Mwajuma Nasombe, taasisi za umma na binafsi pamoja na wanachama wa vilabu mbalimbali vya mazoezi.

Miongoni mwa vilabu vilivyoshiriki ni Wqnafunzi wa Chuo cha Uhasibu (TPS), TK-Movement, Mawenzo Hospital Jogging Club, Rau Forest Jogging Club na RC Jogging Club, huku washiriki wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa mazoezi kama njia ya kujenga taifa lenye wananchi wenye afya na nguvu kazi imara.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.