KOMBA; AHAMASISHA MAZOEZI KUPUNGUZA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba wa (Saba)kutoka kulia wakiwa katika mazoezi ya viungo kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

MOSHI, KILIMANJARO.

WANANCHI wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuzingatia ulaji bora wa vyakula ili kujikinga na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza yanayoendelea kuathiri jamii duniani.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, baada ya kushiriki matembezi ya amani yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi kwa ajili ya maandalizi ya mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Moshi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya matembezi hayo yaliyofanyika Juni 20, 2026, Komba alisema pamoja na kuwa sehemu ya maandalizi ya Mwenge wa Uhuru, matembezi hayo yamelenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa mazoezi katika kuimarisha afya na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani yanaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kupitia mazoezi ya mara kwa mara pamoja na kuzingatia lishe bora inayopunguza matumizi ya chumvi, sukari na mafuta kupita kiasi.

"Kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza duniani. Miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo ni kutofanya mazoezi, kutofuata mlo sahihi pamoja na matumizi makubwa ya chumvi, sukari na mafuta. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua za kujikinga mapema," alisema Komba.

Alisisitiza kuwa wakati umefika kwa jamii kujenga utamaduni wa kujishughulisha na shughuli za kimwili na mazoezi ili kuboresha afya zao na kupunguza gharama za matibabu zinazotokana na magonjwa hayo.

Komba pia aliwataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, akieleza kuwa elimu sahihi ni silaha muhimu katika kupambana na changamoto hiyo.


Aidha, aliipongeza EFM Jogging pamoja na klabu mbalimbali za mazoezi zinazoshiriki mara kwa mara shughuli za kuhamasisha afya kupitia michezo na mazoezi ya viungo, akisema zimekuwa na mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye afya bora.

Katika hatua nyingine, Komba aliwashukuru viongozi wa Manispaa ya Moshi, Kamati ya Usalama ya Wilaya, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wananchi wote walioshiriki matembezi hayo kwa kujitokeza kwa wingi na kuunga mkono kampeni ya kuhamasisha afya kupitia mazoezi.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.