WANANCHI WAHIMIZWA KUSHIRIKI UPANDAJI MITI KULINDA MAZINGIRA

MOSHI-KILIMANJARO.

JAMII imetakiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji miti ili kusaidia utunzaji na uhifadhi wa mazingira, ambayo kwa sasa yanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo mmomonyoko wa udongo na mafuriko.

Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Kiusa Khalid Shekoloa, wakati akizungunza na Kisena Blog, kwenye zoezi la upandaji miti lililofanyika kuzunguka eneo la ofisi ya mtendaji wa Kata ya Kiusa, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Shekoloa amesema miti ina faida nyingi kwa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kuipanda na kuitunza.

“Miti ni tiba, hutoa kivuli, husababisha mvua, huzuia mmomonyoko wa ardhi pamoja na mafuriko. Ni muhimu kuwekeza kwenye upandaji miti ili kuhakikisha mazingira yetu yanabaki salama,” amesema Shekoloa.

Naye Diwani wa Viti Maalum, Renalda Mushi, amewataka wananchi hususan wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa kupanda na kutunza miti, akisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuboresha maisha ya jamii kwa ujumla.

“Utunzaji wa mazingira unaanza na mimi na wewe, tukilinda mazingira leo, tunalinda maisha ya vizazi vijavyo,” amesema Renalda.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiusa, Dativa Tesha, amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi, akibainisha kuwa ushirikiano wa pamoja ndio utakaosaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini.

Amesema kuwa katika kuadhimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM, Kata ya Kiusa imepanda miti 150 kuzunguka maeneo mbalimbali ya kata hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika uhifadhi wa mazingira.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kiusa, Julius Edmund, kwa kushirikiana na Katibu wa CCM Kata ya Kiusa, Yobnesh Maphie, wamesema kuwa utunzaji wa mazingira unaanza na mtu mmoja mmoja, wakihimiza wananchi wote kuchukua hatua sasa ili kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.