CHUO CHA VIWANDA VYA MISITU MOSHI FITI, KUANZISHA MRADI WA MIANZI KWA AJILI YA BIASHARA YA KABONI

MOSHI-KILIMANJARO.

CHUO cha Viwanda vya Misitu (FITI) kiko mbioni kuanzisha mradi wa kilimo cha msitu wa miti aina ya mianzi katika eneo la Kilimanjaro Magharibi, ikiwa ni mkakati wa kunufaika na fursa za biashara ya kaboni.

Hayo yameelezwa Februari 4, 2026, na Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Zacharia Lupala, wakati akitoa mafunzo kuhusu biashara ya kaboni kwa washiriki wa mafunzo ya muda mfupi waliotembelea Kampasi ya FITI iliyopo Kilimanjaro Magharibi.

Dkt. Lupala amesema kuwa kwa sasa misitu ya mianzi imekuwa ikifanya vizuri katika uzalishaji wa carbon credits, hali inayochangia chuo kuona umuhimu wa kuwekeza katika zao hilo lenye tija kiuchumi na kimazingira.

“Kwa sasa misitu ya mimea aina ya mianzi inafanya vizuri sana katika uzalishaji wa carbon credits. Sisi kama chuo tunafikiria kuanzisha msitu wa zao hilo katika eneo hili,” amesema Dkt. Lupala.

Kwa upande wake, mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Yobu Mweleza Kiungo, amekipongeza chuo kwa wazo la kuanzisha msitu wa mianzi, akibainisha kuwa miti hiyo ina manufaa makubwa katika uhifadhi wa mazingira na kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Nakipongeza chuo kwa kuwa na wazo hili, kwani miti aina ya mianzi hufanya vizuri katika uzalishaji wa carbon credits na pia inasaidia utekelezaji wa miradi ya ufugaji nyuki,” amesema Kiungo.

Mafunzo ya muda mfupi kuhusu biashara ya kaboni yanaendelea kutolewa na wakufunzi wabobevu kutoka Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), ambapo leo ni siku ya tatu ya mafunzo hayo, na yanatarajiwa kukamilika tarehe 06 Februari 2026.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.