MOSHI-KILIMANJARO.
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mawenzi imekabidhi vifaa vya kujifungulia kwa akina mama wajawazito katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, vyenye thamani ya shilingi laki tisa.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa niaba ya Kamati ya Siasa ya CCM Mawenzi na Diwani wa Kata hiyo, Apaikunda Naburi, kwa Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo kimkoa yalifanyika Februari 5, mwaka huu katika uwanja wa Manyema.
Tukio hilo lilifanyika wakati mgeni rasmi alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kujionea huduma zinazotolewa hospitalini hapo.
Diwani wa Kata ya Mawenzi Apaikunda Naburi alisema vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na katoni za sabuni za kufulia na kuogea, mama sever pamoja na sabuni za unga, vikiwa na lengo la kuboresha huduma kwa akina mama wanaojifungua.
Naye Afisa Muuguzi msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, Benard Patison, ameishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa wa fedha katika jengo la huduma ya mama na mtoto, akisema uwekezaji huo umeleta msaada mkubwa kwa akina mama wengi wanaofika hospitalini hapo kupata huduma.
“Jengo hili lilikuwapo kwa kipindi kirefu bila kukamilika, lakini mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, aliwezesha kupatikana kwa fedha nyingi zilizosaidia kulikamilisha pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba,” alisema Patison.
Kwa upande wake, Veneranda Massawe, mama mzazi aliyejifungua mtoto wa kiume katika hospitali hiyo, ameishukuru Serikali kwa maboresho ya miundombinu na huduma za afya.
“Huduma hizi hapo awali tulikuwa tunazipata hospitali binafsi, lakini kwa sasa ukifika hospitali ya Mawenzi, unapokelewa vizuri na unapata huduma bora,” alisema Massawe.












