MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, ametenga jumla ya shilingi milioni tano kutoka katika mfuko wake binafsi kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia duni ambao wanashindwa kumudu mahitaji ya msingi ya shule, ikiwemo madaftari, kalamu, sare za shule na chakula cha mchana.
Makoi ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Moshi Vijijini kufanya tathmini ya kina kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wenye mahitaji maalum, ili kubaini wale wasiokuwa na uwezo kabisa wa kumudu mahitaji hayo muhimu ya masomo.
Akizungumza jana na wananchi wa Kata ya Uru Kusini, Mbunge huyo alisema lengo la mpango huo ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili watoto hao zinatatuliwa mapema, ili kuwapa nafasi sawa ya kupata elimu bila vikwazo.
Alisema fedha hizo amezigawa kwa kuzingatia ngazi ya elimu, ambapo shilingi milioni tatu ameziyenga kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari na shilingi milioni mbili kwa wanafunzi wa shule za msingi.
“Baada ya kupokea tathmini ya watoto wenye mahitaji maalum kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji, nitaangalia kata zenye changamoto kubwa zaidi, kisha nitashuka hadi ngazi ya kijiji na kitongoji ili kupata takwimu halisi,” alisema Makoi.
Aliongeza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kabla ya mwezi Machi mwaka huu, watoto wote waliobainika wanakuwa tayari wamepata mahitaji yao ya shule.
Makoi alisema hatua hiyo inalenga kupata takwimu sahihi katika jimbo lenye kata 16, ili msaada uweze kuwafikia walengwa halisi na kwa uwazi.
Katika kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum, Mbunge huyo aliahidi kuendelea kutoa msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kata zote za jimbo hilo.
Alisisitiza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kukosa haki ya elimu kutokana na ukosefu wa mahitaji ya msingi, akisema dhamira yake ni kuona watoto wote wenye sifa ya kusoma wanapata fursa sawa ya elimu bila vikwazo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Uru Kusini, Fredrick Mbararia, aliwasilisha changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo, zikiwemo ubovu wa barabara ya Mama Ndizi, tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na uchakavu wa Shule ya Msingi Mrupanga.
Akijibu changamoto hizo, Mbunge Makoi alisema tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Mama Ndizi, hivyo kero hiyo inatarajiwa kuisha. Kuhusu maji, alisema mabomba tayari yameshawasili na tatizo hilo linakwenda kutatuliwa muda si mrefu.
Kuhusu uchakavu wa Shule ya Msingi Mrupanga, alisema ataliwasilisha bungeni ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua za ukarabati au ujenzi upya wa miundombinu ya shule hizo zilizojengwa miaka mingi iliyopita na kwa sasa zimechakaa.








