MWANGA-KILIMANJARO.
KATIBU wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ambaye pia ni Mlezi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Rabia Abdallah Hamid, amempongeza Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kyu6y7ambarage Nyerere, kwa kuweka misingi imara iliyoifanya Tanzania kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano hadi leo.
Rabia aliyasema hayo Februari 3,2026 wilayani Mwanga, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mkoa. Katika ziara hiyo, alitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt. Asha-Rose Migiro, na kukagua bweni lililokumbwa na janga la moto, ambalo lilikuwa likiwaweka wanafunzi 347 wa kidato cha kwanza hadi cha tatu.
Akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule hiyo, Rabia alisema misingi iliyoachwa na waasisi wa taifa ni amani, upendo na mshikamano, huku akisisitiza kuwa msingi mkuu wa uongozi ni kuwatumikia wananchi, jambo ambalo Hayati Mwalimu Nyerere alilisimamia kikamilifu.
Alieleza kuwa waasisi wa taifa akiwemo Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, waliwahi kuwa wanafunzi kama walivyo wanafunzi wa sasa, kabla ya kuja kuwa viongozi wa taifa kutokana na misingi bora iliyojengwa tangu awali.
“Misingi ya nchi yetu inamjenga kila mmoja kuwa kiongozi wa taifa hili. Nawasihi msome kwa bidii ili muweze kufikia malengo yenu ya kuwa viongozi wa kuwatumikia Watanzania,” alisema Rabia.
Aliongeza kuwa hakuna kosa kubwa kama kuharibu tunu za taifa, akibainisha kuwa ndiyo sababu Mwalimu Nyerere alifuta siasa za mgawanyiko kama udini, ukabila na matabaka ya kijamii.
“Haijalishi unatoka mkoa gani, familia gani au tabaka gani, Mwalimu Nyerere aliyafuta yote hayo,” alisisitiza.
Aidha, Rabia ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, alisema hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatokani na familia maarufu au yenye nguvu za kiuchumi, bali amefanikiwa kwa misingi ya taifa, maono na juhudi binafsi.
Aliwataja pia viongozi wengine akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Emanuel Nchimbi na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akisema wote walikuwa na maono yaliyowawezesha kufikia nafasi walizonazo sasa za kuwatumikia wananchi.
Rabia aliwataka wanafunzi kote nchini kutojikatia tamaa, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayezaliwa akiwa kiongozi, bali kila mmoja ana nafasi ya kuwa kiongozi endapo atajiandaa ipasavyo.
Kwa upande mwingine, alisema Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, akitaja kuanzishwa kwa mpango maalum wa KKK, unaolenga kuwaandaa vijana kuwa viongozi wa baadaye wa taifa.











