ALAT Kilimanjaro yatoa ufafanuzi kuhusu clip Iliyodai kumdharirisha Mbunge Dk. Mathayo

MOSHI-KILIMANJARO.

KATIBU wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) mkoa wa Kilimanjaro, Shadrack Mhagama, ametoa ufafanuzi kuhusu clip ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kumdharirisha Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, Dk. David Mathayo.

Akizungumza na vyombo vya habari Januaria 31,2026 ofisini  kwake Mhagama alisema kuwa Januari 30, mwaka huu, ALAT mkoa wa Kilimanjaro ilifanya mkutano mkuu maalum wa uchaguzi uliolenga kupata wawakilishi mbalimbali kutoka miongoni mwa wajumbe wake ambao ni madiwani walioteuliwa kutoka kila halmashauri.

Alisema kuwa katika mkutano huo, wajumbe pia walitakiwa kupendekeza majina ya wabunge watakaowakilisha ALAT mkoa wa Kilimanjaro katika shughuli mbalimbali za kibunge, ambapo ilipaswa kupatikana mbunge mmoja wa uwakilishi.

Mhagama, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, alisema kuwa katika kikao hicho wajumbe katika kupendekeza majina ya wabunge mkoa wa Kilimanjaro,  mbunge wa Jimbo la Same Magharibi Dk. David Mathayo,  alitajwa pamoja na wabunge wengine wa Mkoa wa Kilimanjaro

“Katika kikao hicho, mjumbe mmoja alipendekeza jina la Dk. David Mathayo, huku wajumbe wengine wakipendekeza majina ya Ibrahim Shayo na Morris Makoi,” alisema Mhagama.

Alifafanua kuwa majina hayo yalipendekezwa na wajumbe wa mkutano huo na siyo kwamba wabunge husika walikuwa wanagombea au kushindana kwa nafasi hiyo, kwani hakuna mbunge aliyeshiriki kikao hicho wala kufanya kampeni za kuomba nafasi hiyo ya uwakilishi.

Mhagama alikiri kuwa kauli iliyosikika kwenye clip ya video iliyosambaa mitandaoni ikimtaja Dk. David Mathayo kuwa alipata kura moja kati ya kura 28 haikuwa sahihi, kwani mbunge huyo hakuomba nafasi hiyo, hakugombea wala kufanya kampeni yoyote.

“Haipaswi kuonekana kama tumemdhalilisha mbunge wetu kwa kupigiwa na kupata kura moja. Jina lake lilipendekezwa tu na wajumbe, kama ilivyokuwa kwa wabunge wengine,” alisisitiza Mhagama.

Kutokana na hilo, Mhagama ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, amemuomba radhi Mbunge Dk. David Mathayo kwa usumbufu uliosababishwa na clip hiyo kwa wananchi wa jimbo lake, kwake binafsi na kwa umma kwa ujumla.

Katika mkutano huo wa Januari 30, ALAT mkoa wa Kilimanjaro pia ilifanya uchaguzi wa viongozi wake, ambapo Gilbert Tarimo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Kilimanjaro, huku Yusto Mapande akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.

Nafasi za wajumbe wa Kamati tendaji zilichukuliwa na Samwel Mmari, Fredrick Mbararia Mushi na Juma Raibu, huku nafasi za Wasemaji wa ALAT mkoa zikichukuliwa na Aisha Gogo na Jenipher Nyambo.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.