MOSHI-KILIMANJARO.
JUMUIYA ya Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini imewakumbuka na kuwathamini waasisi wanawake wa jumuiya hiyo waliokuwepo tangu enzi za vyama vya ASP na TANU hadi kuungana na kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977.
Waasisi hao ni miongoni mwa wanawake mashujaa walioshuhudia na kushiriki kwa vitendo katika harakati za kuunganisha vyama vya ASP na TANU, hatua iliyosababisha kuzaliwa kwa CCM, chama tawala nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, alisema jumuiya hiyo imeona umuhimu wa kuwaungana na waasisi hao kwa kuwapatia misaada mbalimbali ya kijamii kama ishara ya kuwathamini kwa mchango wao mkubwa kwa taifa na chama.
Alisema misaada hiyo imejumuisha sukari, mafuta ya kula, sabuni za kufulia na kuogea pamoja na kushiriki nao chakula na vinywaji, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika Februari 5, 2026.
“Hawa ni watangulizi wetu na waasisi wetu wanawake wa UWT walioshuhudia kuungana kwa vyama vya ASP na TANU na kuzaliwa kwa CCM. Tukiwa tunaelekea kuadhimisha miaka 49 ya CCM, tumeona ni vyema kuwatembelea na kuwashika mkono kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu kama ishara ya kuendelea kuwathamini katika utumishi wao,” alisema Komba.
Baada ya zoezi hilo, Mwenyekiti huyo aliambatana na Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya pamoja na madiwani wanaotokana na jumuiya hiyo, ambapo walitembelea Zahanati ya Njoro, kufanya usafi wa mazingira na kupanda miti ya kivuli na matunda kuzunguka eneo la zahanati hiyo.
Katika ziara hiyo, Komba aliipongeza Serikali kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika Zahanati ya Njoro, akisema uwekezaji uliofanywa katika miundombinu na vifaa tiba utaongeza ufanisi wa huduma za afya kwa wananchi.
“Kata ya Njoro tumeshuhudia uwekezaji mkubwa katika majengo na vifaa tiba vilivyopo katika zahanati hii. Maboresho haya yatasaidia kwa kiasi kikubwa akinamama wajawazito waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya kujifungua,” aliongeza.
Aidha, Komba alimpongeza Diwani wa Kata ya Njoro ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Abdallah, kwa juhudi zake katika kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum, Joyce Ndossi, alisema Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha sekta ya afya kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa kwa ujumla.