MBUNGE JIMBO LA MOSHI VIJIJINI, MORRIS MAKOI, AKABIDHI GARI LA WAGONJWA KITUO CHA AFYA URU KUSINI

Mbunge Jimbo la Moshi Vijijini Morris Makoi, akimkabidhi funguo za gari la wagonjwa mtaala wa maabara kituo cha afya Uru Kusini Dk. Pius Ngongwa.

MOSHI-KILIMANJARO 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetoa gari la wagonjwa kwa Kituo cha Afya Uru Kusini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni jitihada za kuimarisha huduma za afya na kurahisisha rufaa za dharura kwa wagonjwa wanaohitaji huduma katika Hospitali ya Wilaya au Mkoa.

Gari hilo limekabidhiwa Januari 31,2026 na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, ambaye alisema kuwa utoaji wa gari hilo ni utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan, kwa vitendo.

Makoi alisema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni yaliyo mbali na hospitali za wilaya na mkoa, ili nao wapate huduma bora za afya kwa wakati.

“Serikali inatekeleza ahadi zake kwa vitendo, gari hili ni sehemu ya mkakati mkubwa wa kuondoa kero za wananchi na kuboresha huduma za afya,” alisema Makoi.

Aidha, alisisitiza kuwa gari hilo litatumika kusafirisha wagonjwa bila malipo yoyote, huku akiwataka watumishi wa afya pamoja na viongozi wa Serikali ngazi ya kijiji na kata ya Uru Kusini kuhakikisha gari hilo linatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na linatunzwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Uru Kusini, Dk. Alex Sabinus, alisema kuwa gari hilo litarahisisha rufaa za dharura kwenda hospitali za wilaya na mkoa, na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya uzazi kwa kuwahi kuwafikisha hospitalini kina mama wajawazito.

Dk. Sabinus aliongeza kuwa uwepo wa vifaa vya kitabibu ndani ya gari hilo utawawezesha wagonjwa kupata huduma za awali wakiwa njiani, jambo litakalopunguza adha na gharama ambazo awali wananchi walilazimika kuzibeba kwa kukodi magari ya kiraia.

Aliahidi kuwa gari hilo litatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Halmashauri itahakikisha linafanyiwa matengenezo ya kitaalamu na kwa wakati ili lidumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hata hivyo, Dk. Sabinus alibainisha kuwa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa miundombinu nje ya majengo, hususan katika majengo ya RCH na nyumba za watumishi, uhaba wa watumishi wa afya kutokana na ikama, pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara hasa kipindi cha mvua, hali inayosababisha utoaji wa huduma kuzorota.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitandu, Kata ya Uru Kusini, Elipid Cassimiri, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya siku 100 za awali, akisema upatikanaji wa gari hilo ni ushahidi wa dhamira ya serikali katika kuimarisha sekta ya afya.

Naye Diwani wa Kata ya Uru Kusini, Fredrick Mbararia, alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, kwa kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa vifaa tiba, magari ya wagonjwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya jimbo hilo.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutoa gari hilo ambalo litakwenda kuokoa maisha ya wananchi, hususan kina mama wajawazito wanaopewa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya au hospitali za rufaa.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.