HALMASHAURI, MANISPAA MKOA WA KILIMANJARO ZATAKIWA KUTENGA FEDHA KWA AJILI YA MFUKO WA ALAT MKOA, TAIFA

MOSHI-KILIMANJARO.

HALMASHAURI zote za mkoa wa Kilimanjaro zimetakiwa kuweka vifungu maalum katika bajeti ya mwaka wa fedha elfu mbili ishirini na sita hadi elfu mbili ishirini na saba, kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania, ALAT, ngazi ya mkoa na taifa.

Wito huo umetolewa Januari  30,2026 na Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Kilimanjaro, Gilbert Tarimo, mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu maalum wa uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo uliofanyika mkoani humo.

Tarimo amesema kwa muda mrefu baadhi ya halmashauri hazikuwa zikitenga fedha kwa ajili ya ALAT, hali iliyokuwa ikikwamisha utekelezaji wa majukumu ya jumuiya hiyo.

Amesisitiza kuwa katika bajeti ijayo, halmashauri zote za mkoa na manispaa zinapaswa kuweka vifungu hivyo ili ziweze kuchangia mfuko wa ALAT mkoa na taifa.

Amesema pia kuna changamoto mbalimbali katika halmashauri za mkoa wa Kilimanjaro, ikiwemo upungufu wa watumishi katika sekta tofauti, changamoto ambazo ALAT itazifikisha serikalini kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Aidha, Tarimo amesema bado kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo haijakamilika katika halmashauri mbalimbali, akieleza kuwa moja ya majukumu ya ALAT ni kutembelea, kukagua na kushauri juu ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema ALAT itabaini changamoto zilizopo katika usimamizi au matumizi ya fedha na kutoa ushauri ili miradi ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, kulingana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Kilimanjaro, Yusto Mapande, amesema jukumu kubwa la jumuiya hiyo ni kutetea na kusimamia maslahi ya viongozi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha yanatekelezwa kwa tija.

Ameongeza kuwa majukumu waliyopewa na serikali kuu pamoja na wananchi yatasimamiwa kwa ufanisi, huku wakihakikisha malengo ya taasisi hiyo yanafikiwa.

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Cedrick Pangani, amesema wataungana kwa nguvu kuhakikisha halmashauri zote zinapitisha vifungu vya bajeti kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa ALAT mkoa na taifa, akisisitiza kuwa kifungu hicho ni muhimu kwa ustawi wa jumuiya hiyo.

Wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi, Mwenyekiti wa kikao hicho John Meela, alimtangaza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rombo, Gilbert Tarimo, kuwa Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Kilimanjaro, huku Yusto Mapande akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.

Aidha, Ibrahim Shayo amechaguliwa kuwa mwakilishi wa wabunge katika ALAT mkoa, wakati wajumbe wa Kamati Tendaji wakiwa ni Samwel Mmari, Fredrick Mushi na Juma Raibu. Nafasi za Wasemaji wa ALAT mkoa zimechukuliwa na Aisha Agogo na Jenipher Nyambo.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.