MOSHI-KILIMANJARO.
JUMUIYA ya Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi Manispaa ya Moshi imefanya ziara ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa mkoa huo.
Akizungumza Januari 27,2926, wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa UWT Manispaa ya Moshi, Theresia Komba, amesema jumuiya hiyo imeridhishwa na maboresho makubwa yaliyofanywa katika hospitali hiyo, hususan Jengo la Mama na Mtoto pamoja na vitengo vingine muhimu vya tiba.
Alisema walitembelea na kujionea uwekezaji uliofanyika katika Kitengo cha Dharura, Uangalizi Maalumu (ICU), Radiolojia ikiwemo CT-Scan, Uangalizi wa Watoto Wachanga (NICU), Wodi ya Upasuaji pamoja na Kitengo cha Kusafisha Figo.
Alisema kupatikana kwa huduma za kibingwa ndani ya Hospitali ya Mawenzi kumepunguza adha kwa wananchi wa Kilimanjaro, ikiwemo kusafiri umbali mrefu, gharama za matibabu na muda wa kufuata huduma, kwani sasa huduma hizo zinapatikana ndani ya mkoa.
Katika ziara hiyo, UWT pia walitembelea wodi ya wazazi na kukabidhi zawadi mbalimbali kwa akinamama waliolazwa, ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha afya ya mama na mtoto.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mawenzi, Dk. Abilah Issa, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto na uwekezaji wa shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha hewa tiba, hatua iliyosaidia hospitali kujitegemea.
Akizungumzia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Dk. Issa alisema hospitali tayari imejipanga kuanza kupokea makundi mbalimbali yakiwemo wazee, watu wenye ulemavu na wajawazito kwa lengo la kuwapatia huduma bora na vipimo stahiki.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk. Victor Adolph, alisema walihamia katika Jengo la Mama na Mtoto Novemba mwaka jana, na tangu wakati huo wamewahudumia akina mama wajawazito 456, ambapo 230 walijifungua kwa njia ya kawaida na 226 kwa njia ya upasuaji.
Mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Moshi, Ovena Kowero, amesema ameridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya, na kuahidi kuwa balozi wa kuisemea vyema Serikali kwa wananchi wengine.

















