MOSHI-KILIMANJARO.
CHUO cha Viwanda vya Misitu Moshi, FITI, kimetajwa kuwa taasisi kinara nchini katika kuzalisha wataalamu wa sekta ya viwanda vya misitu, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya watumishi wanaofanya kazi katika sekta hiyo nchini Tanzania ni wahitimu wa chuo hicho.
Akizungumza Januari 27,2026 na waandishi wa habari chuoni hapo, Mkuu wa Chuo cha FITI, Dk. Zacharia Lupala, amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 40 ya watendaji wanaofanya kazi mashambani katika sekta ya misitu ni wahitimu wa FITI na wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na mfumo mzuri wa ufuatiliaji wa wahitimu pamoja na mbinu za ufundishaji zinazozingatia vitendo, ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa inayotolewa na wakufunzi waliobobea.
Ameongeza kuwa asilimia 20 ya wahitimu wa FITI wameanzisha makampuni yao binafsi katika sekta ya viwanda vya misitu, jambo linalochangia kukuza uchumi na kutoa ajira kwa Watanzania.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya misitu, akisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, bajeti ya kuendeleza mafunzo chuoni hapo imeongezeka kutoka shilingi milioni 260 hadi shilingi milioni 480, huku asilimia 50 ya wanafunzi wakipata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Alisema chuo cha FITI kina jukumu la kuwajengea vijana ujuzi wa kupanda, kutunza na kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu ili waweze kujiajiri au kuajiriwa, huku akisisitiza kuwa upandaji miti ni suluhisho la changamoto za ajira, kipato na mazingira.
Kwa upande wao, wanafunzi wa chuo hicho akiwemo Abiud Ayubu na Pendo Ami, walisema mafunzo wanayopata yanawawezesha kuchakata mazao ya misitu na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutumia misitu kwa maendeleo ya jamii.












