WAHITIMU UMBWE SEKONDARI WATAKIWA KUTUMIA ELIMU KAMA CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA

MOSHI-KILIMANJARO.

WAHITIMU wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Umbwe wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya kuleta maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa jana na Diwani wa Kata ya Pasua, Barreh Ally Farrah, wakati wa mahafali ya kwanza ya dini ya Kiislamu tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu Umbwe (UMUSA), yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule hiyo.

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 57 wa dini ya Kiislamu wanatarajiwa kuhitimu masomo yao ya kidato cha sita Mei mwaka huu.

Akizungumza kama mgeni rasmi, Barreh aliwataka vijana hao kutumia elimu yao kikamilifu katika kuijenga nchi, hususan kuelekea uchumi wa kati kupitia sekta za viwanda, kilimo na ufugaji.

"Kama vijana, nendeni mkaitumie elimu mliyoipata kama chachu ya kuleta maendeleo ya Taifa. Tunategemea kupata wataalamu mbalimbali wakiwemo marubani, wanasiasa, wahandisi na madaktari ambao watalisaidia Taifa letu kupiga hatua za kimaendeleo,” alisema Barreh.


Aidha, aliwataka vijana wa dini ya Kiislamu kuwa wazalendo na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukuza uchumi wa nchi kupitia sera ya viwanda, akisisitiza kuwa wao ndio tegemeo la Taifa la sasa na baadaye.

Pia aliwahimiza kutumia vyema fursa zilizopo za kimaendeleo na kuwa sehemu ya kutafuta suluhu ya changamoto zilizopo nchini, huku akiwataka kutumia simu za mkononi kwa ajili ya kujifunza na kuacha matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayochochea migogoro na vurugu.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wanafunzi na Vijana wa Kiislamu Tanzania (TAMSYA) mkoa wa Kilimanjaro, Abdulkareem Nzogera, aliwasihi vijana kuyaishi na kuyatenda yale yote waliyokuwa wakifundishwa shuleni hata wanapokuwa katika jamii.

“Niwasihi vijana wa Kiislamu kuwa na tabia njema, kujiepusha na makundi mabaya ya rika na kuwa mfano bora katika jamii ya Watanzania,” alisema Nzogera.

Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za jamii na siyo chanzo cha vurugu.

Naye Mwenyekiti wa Idara ya Vijana wa Kiislamu mkoa wa Kilimanjaro, Athuman Mayeye, alisema vijana wengi wamekuwa wakisoma kwa matumaini ya kuajiriwa serikalini, hali inayowafanya kuwa tegemezi pindi wanapokosa ajira rasmi.

“Takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Kilimanjaro kuna zaidi ya wahitimu takribani laki moja kutoka vyuo vikuu kila mwaka, lakini wengi wao hujikuta wakifanya kazi zisizo rasmi nje ya taaluma walizosomea,” alisema Mayeye.

Awali, Mwalimu wa Malezi wa Shule ya Sekondari Umbwe, Ally Said Mwalimu, alisema jukumu la mzazi au mlezi ni kuhakikisha wanafunzi wanalelewa katika misingi ya maadili mema, ikiwemo ya dini ya Kiislamu.

Aliwataka wanafunzi kufuata sheria na taratibu za shule ili kujiepusha na kuharibu ndoto zao za baadaye.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Ridhiwani Makame alisema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa zulia la kuswalia, mikeka kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, upungufu wa Mas-haf na vitabu vya kujifunzia, kabati la kuhifadhi vitabu pamoja na kifaa cha intaneti kwa ajili ya kujifunza masomo ya kompyuta.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.