MOSHI-KILIMANJARO
TAASISI ya Kijana Kwanza iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imekabidhi rasmi jengo la wodi ya mama wajawazito pamoja na vifaa tiba vya kisasa kwa Zahanati ya Njoro, ikiwa ni sehemu ya mchango wake wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa jengo la mama na mtoto, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo, Mujibu Abeid, alisema taasisi imetoa shilingi milioni 125 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama wajawazito pamoja na shilingi milioni 75 kwa ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
Alisema vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia, vitanda vya upasuaji na vifaa vya ufuatiliaji wa wagonjwa, huku akisisitiza kuwa lengo lao ni kuhakikisha miundombinu hiyo inatoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Njoro ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, aliishukuru Taasisi ya Kijana Kwanza kwa mchango mkubwa uliobadilisha taswira ya Zahanati ya Njoro.
Alisema ujenzi wa wodi hiyo umetokana na jitihada za kuwasilisha changamoto zinazowakabili akinamama wajawazito, huku akibainisha kuwa awali taasisi hiyo pia ilishiriki kukarabati zahanati iliyokuwa imechakaa.
Kidumo alisema kukamilika kwa wodi hiyo kumeondoa adha kwa akinamama waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kujifungua katika kata jirani, na kuongeza kuwa wodi hiyo ina uwezo wa kuhudumia akinamama 10 kwa wakati mmoja na imepatiwa mashine ya Ultrasound.
Aidha, aliahidi kutoa shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya bima ya afya kwa familia 10 kutoka kaya maskini pamoja na kugharamia vifaa vya kujifungulia kwa akinamama 50, huku akiomba Manispaa ya Moshi kupanua eneo la zahanati ili kuongeza wodi nyingine.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Moshi, Dk. Erick Atugonza, alisema ujenzi wa wodi hiyo ulianza Agosti 2024 na kwamba Zahanati ya Njoro inahudumia wananchi wapatao 12,252 kwa mwaka wakiwemo akinamama wajawazito 1,796, huku wananchi wakipongeza ushirikiano huo na kuutaja kuwa mfano wa kuigwa katika kuboresha huduma za afya.
.jpg)

.jpg)

.jpg)
.jpg)

.jpg)
