SHAYO AKABIDHI VIFAA KWA VIJANA 30 WA VETA MOSHI, ATOA WITO “NENDENI MKASOME”

MOSHI-KILIMANJARO.

MBUNGE wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amewataka vijana kutumia fursa ya elimu ya ufundi kujijengea maisha bora ya baadaye, akisisitiza kuwa hilo ndilo azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuona kila Mtanzania mwenye sifa anapata elimu.

Shayo alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi vifaa vya shule kwa vijana 30 aliowafadhili kusoma katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kwa kipindi cha miaka mitatu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wakati wa kampeni.

“Nendeni mkasome. Taifa linahitaji wataalamu wabobezi katika nyanja mbalimbali. Nyie ni watu muhimu sana katika ujenzi wa nchi hii,” alisema Shayo.

Aliongeza kuwa ni furaha kwake kuona vijana hao 30 atakaowagharamia masomo kwa miaka mitatu wanamaliza kwa mafanikio na kuajiriwa katika taasisi za umma na binafsi.

“Nitafurahi sana kusikia vijana niliowasomesha wote wamemaliza masomo yao na wanafanya kazi katika maeneo mbalimbali. Nendeni mkawa waaminifu na waadilifu, tambueni mnakwenda kusoma kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye na familia zenu,” alisisitiza.

Mbunge huyo pia aliwataka wabunge wengine kuona umuhimu wa kusaidia vijana katika majimbo yao kupata elimu ya ujuzi ili kupunguza utegemezi na kuongeza ajira kwa vijana.

Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge, Samwel Kamandwa, alisema walipokea maombi 360 kutoka vijana wa kata 21 za Manispaa ya Moshi, na kisha kuendesha mchakato wa usaili kwa kuzingatia vigezo vya VETA.

“Baada ya kukamilisha mchakato wa uchambuzi, tulibaki na vijana 30 waliokidhi vigezo vya kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi. Mbunge atagharamia ada na michango yote inayotakiwa chuoni hapo kwa kipindi chote cha miaka mitatu,” alisema Kamandwa.

Aliongeza kuwa mbali na kulipiwa ada, wanafunzi hao wamekatwa bima ya afya kwa kipindi chote watakachokuwa chuoni, pamoja na kununuliwa mahitaji muhimu ya masomo ikiwemo madaftari, kalamu, kompasi, mabegi na vifaa vingine vinavyohitajika.

Baadhi ya wanufaika wa ufadhili huo, akiwemo Debora Nko, George Mwita na Yusuph Mdee, walimshukuru Mbunge Shayo kwa msaada huo, wakisema bila ufadhili huo wasingeweza kuendelea na masomo kutokana na hali za kifamilia.

“Kwa kweli tusingeweza kusoma kutokana na uwezo mdogo wa familia zetu. Umetupigisha hatua kubwa sana. Tunakuahidi tutasoma kwa bidii na kufanya vizuri,” walisema.





Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.