MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo, amesema moja ya mafanikio makubwa anayojivunia katika kipindi chake chote cha ubunge ni kushiriki kikamilifu kupitisha sheria inayolinda wagombea wanawake dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia wakati wa kampeni za uchaguzi.
Tarimo alitoa kauli hiyo Februari 14, 2026, alalipohutubiWajumbe wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) katika kikao cha kawaida cha Baraza la UWT Wilaya ya Moshi Mjini, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema kabla ya kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo, vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wagombea wanawake vilikuwa havitambuliwi kama kosa la uchaguzi, hali iliyosababisha wanawake wengi kukosa haki ya msingi ya kulalamikia matokeo pale walipokuwa wameathiriwa na vitendo hivyo.
“Sheria tuliyoipitisha sasa inatambua udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wagombea wanawake kama siyo tu kosa la jinai, bali pia ni kosa la uchaguzi. Hivyo, kama mgombea atashinda kwa mazingira ya kumdhalilisha mpinzani wake kwa misingi ya kijinsia, ushindi wake unaweza kutenguliwa mahakamani endapo ushahidi utathibitishwa,” alisema Tarimo.
Alikumbusha uzoefu wake wa mwaka 2010 alipogombea udiwani katika Manispaa ya Moshi kupitia Kata ya Kilimanjaro, ambapo wagombea wanawake wa CCM walikumbana na vitisho na matusi ya kijinsia wakati wa kampeni.
“Wakati huo, udhalilishaji wa kijinsia haukuwa kosa la uchaguzi. Hukuweza kwenda mahakamani kupinga matokeo kwa sababu umetukanwa au kudhalilishwa kwa misingi ya jinsia yako,” alieleza.
Kwa mujibu wa Tarimo, marekebisho hayo ya sheria yalifanyika kwa juhudi za wabunge waliotambua umuhimu wa kuwalinda wanawake katika siasa, na yeye alikuwa miongoni mwa waliosimama kidete kuhakikisha sheria hiyo inapita ili kuimarisha usawa na haki katika mchakato wa uchaguzi.







