MOSHI-KILIMANJARO.
WAJUMBE wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi, wamepongezwa kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kata wanazotoka, ambayo imechangia ushindi wa asilimia 97 wa Rais wa Samia Suluhu Hassan.
Hayo yalisemwa Januari 24,2026 na Mwenyekiti wa (UVCCM), Uvenari Shirima, wakati akifungua kikao cha Baraza la UVCCM kilichofanyika katika Ofisi za CCM Wilayani humo.
"Hatuwezi kuacha kuzungumzia mafanikio ya Chama cha Mapinduzi bila kuwataja kundi la UVCCM, kuanzia ngazi ya matawi, kata, wilaya hadi mkoa, ambao ndiyo wa walichangia kuwapa ushindi wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo ya Urais, Wqbunge na Madiwani,"alisema Shirima.
Alisema vijana wa CCM walikuwa mstari wa mbele katika kusaka kura za Rais Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani, hatua iliyosaidia kukihakikishia chama ushindi mkubwa katika chaguzi mbalimbali.
Shirima alisema kuwa vijana wana jukumu kubwa la kulinda na kuendeleza amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi, jambo litakalosaidia CCM kuendelea kushika dola kwa misingi ya demokrasia na maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Same, Azza Karisha, aliwataka vijana kujiimarisha kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha, aliwaomba madiwani waliochaguliwa kupitia kundi la vijana kuhakikisha wanawasimamia na kuwasaidia vijana kupata fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana serikalini, ikiwemo mikopo na miradi ya maendeleo kwa vijana.
Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Moshi, Melkiori Pandaleo, alisema kikao hicho cha Baraza la UVCCM, kililenga kupanga mikakati ya kusonga mbele, ikiwemo kuimarisha umoja wa vijana, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
"Kikao hiki cha Baraza la UVCCM ni kikao cha kawaida chenye lengo la kujadili mipango mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya vijana katika wilaya ya Moshi, tunalenga kuona vijana wanapiga hatua za kiuchumi."alisema Pandaleo.
Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, hivyo ni muhimu vijana kuchangamkia fursa hizo.















