RT YAPENDEKEZA KUANZISHWA KWA MBIO ZA WATOTO KILIMANJARO MARATHON

MOSHI-KILIMANJARO.

WAANDAAJI na Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon wametakiwa kuanzisha mbio maalum za watoto zitakazokuwa na udhamini, ili kusaidia kuibua na kuandaa vipaji vya wakimbiaji chipukizi kwa mashindano makubwa ya baadaye.

Wito huo umetolewa Januari 23, 2026 Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) Mkoa wa Kilimanjaro, Nelson Mrashan, wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon msimu wa 24 zitakazofanyika Machi 22 mwaka huu.

Mrashan amesema watoto wengi wamekuwa wakijitokeza kushiriki mbio za kilometa tano, hali inayoonesha kuwepo kwa vipaji vingi vinavyohitaji kuandaliwa mapema kupitia mbio maalum zitakazokuwa chini ya udhamini.

Aidha, amewapongeza waandaaji na wadhamini wa mashindano hayo kwa kuendelea kuyaboresha kila mwaka, huku akibainisha kuwa Chama cha Riadha Tanzania kitaendelea kutoa ushirikiano na ushauri.

Amesema pia RT ipo katika maandalizi ya kuweka kambi ya miezi miwili kwa ajili ya kuwaandaa wakimbiaji wasiopungua kumi, akisisitiza kuwa Kilimanjaro Marathon iwe kipimo cha maandalizi ya mashindano makubwa ya kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Madola na Olimpiki.

Aidha, amewashukuru waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kuyatangaza mashindano hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003, ambapo kwa sasa hushirikisha zaidi ya washiriki elfu kumi na tatu kutoka nchi zaidi ya sitini duniani.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.