MOSHI-KILIMANJARO.
MBIO za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon zimeendelea kuwa chachu ya kuitambulisha Tanzania katika medani za kimataifa, sambamba na kukuza utalii wa Mkoa wa Kilimanjaro kupitia dhana ya utalii wa michezo.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Michezo wa Mkoa huo, Anthony Ishumi, wakati wa uzinduzi wa msimu wa 24 wa mbio hizo maarufu zinazotarajiwa kufanyika mwaka 2026, hafla iliyofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Nzowa alisema mbio hizo zimekuwa kivutio kikubwa cha utalii, huku wageni kutoka mataifa mbalimbali wakitumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ikiwemo Hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro, visiwa vya Zanzibar pamoja na kupanda Mlima Kilimanjaro.
“Sote tunajua jinsi Kilimanjaro International Marathon imekuwa ikikuza utalii wa Mkoa kupitia dhana ya utalii wa michezo,” alisema Nzowa.
Aliongeza kuwa tukio hilo huvutia zaidi ya washiriki 13,000 pamoja na idadi kubwa ya watazamaji kutoka zaidi ya nchi 60, hatua inayolifanya kuwa tukio kubwa na kongwe zaidi la mbio za marathon nchini Tanzania, hasa likizingatiwa kuwa linaadhimisha miaka 24 ya mafanikio mfululizo.
Kwa kutambua mchango wa wadau, Nzowa aliwapongeza wadhamini wa mbio hizo wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager, pamoja na YAS na Benki ya CRDB.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza wadhamini wote kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha mafanikio ya tukio hili,” alisema.
Aliwataja wadhamini wengine kuwa ni pamoja na Kilimanjaro Water, TPC Sugar, GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement, Harleys Healthcare Solutions na ALAF Limited, pamoja na hoteli za Salinero, Kibo Palace Arusha na Keys Hotel Moshi.
Aidha, aliwashukuru waonyeshaji wa bidhaa mbalimbali na kuwasihi washiriki na wageni kutembelea mabanda yao ya maonyesho, akiwataja kuwa ni pamoja na HiSense, The Rwenzori Marathon, Schultz Sportreisen, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Healthcare, Enson Africa Chartered Accounting, Nyikani Trails, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Graph X.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Masoko wa Tanzania Breweries Limited (TBL), Khensani Mkhombo, alisema kampuni hiyo inajivunia kuendelea kudhamini mbio hizo kupitia chapa yake ya Kilimanjaro Premium Lager kwa kipindi cha miaka 24 tangu kuzinduliwa kwake rasmi.
“Mbali na kukuza michezo, tukio hili limekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii na kulitambulisha Taifa letu kimataifa,” alisema Mkhombo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa YAS, Shaibu Hamisi, alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa mdhamini rasmi wa Kilimanjaro International Half Marathon kwa mwaka wa 11 mfululizo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya kampuni katika kuunganisha na kuwezesha jamii kote nchini.
Naye Meneja wa Biashara wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Emanuel Kafui, alisema benki hiyo imeamua kudhamini mbio za CRDB 5km Fun Run kutokana na mchango mkubwa wa tukio hilo katika kuunganisha jamii na kukuza uchumi wa taifa kupitia utalii wa michezo.
Marathon ya Kimataifa ya Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) tarehe 22 Machi, 2026, ikiandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited kwa uratibu wa kampuni ya Executive Solutions, huku Wild Frontiers wakihusika na usafiri wa ndani na masoko ya kimataifa ya tukio hilo.