MOSHI-KILIMANJARO.
Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) Dk. Zacharia Lupala, akipanda mti katika chuo hicho kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za uhifadhi wa mazingira.
CHUO cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) kimepanda miti zaidi ya 100 kuzunguka eneo la chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha ulinzi wa mazingira kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Akizungumza Januari 27, 2026 wakati wa zoezi hilo la upandaji miti, Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Zacharia Lupala, alisema FITI imeamua kuungana na Watanzania wengine kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais Samia kwa vitendo kupitia utunzaji wa mazingira.
Alisema zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Kauli mbiu isemayo “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti,” ambapo chuo hicho kinajivunia kushirikiana na wanafunzi na wakufunzi wake katika kupanda miti kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia.
“Tumepanda miti hii ili kuendelea kutunza mazingira yetu na pia kupata faida nyingine mbalimbali ikiwemo kivuli, matunda, hewa safi, mvua za kutosha pamoja na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dk. Lupala.
Aliongeza kuwa utunzaji wa mazingira una mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo FITI kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wote imeunga mkono kikamilifu jitihada za Rais Samia hususan katika suala la upandaji miti.
Dk. Lupala alisisitiza kuwa ili kukabiliana na tatizo la ujangwa, Watanzania wanapaswa kuendelea kupanda miti kwa wingi ili kuhakikisha nchi inakuwa sehemu ya kueneza ukijani badala ya kueneza ujangwa.
Kwa upande wao, baadhi ya wakufunzi na wanafunzi wa chuo hicho akiwemo Pendo Ami na Abiud Ayubu Ntula, walilipongeza zoezi hilo wakisema litaboresha mazingira ya chuo pamoja na jamii inayokizunguka
![]() |









