MOSHI-KILIMANJARO.
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imenunua na kusimika mtambo mpya wa kisasa wa kutibu mbao katika Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), hatua inayolenga kuimarisha mafunzo ya vitendo na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya misitu.
Akizungumza chuoni hapo, Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Dkt. Zacharia Lupala, ameipongeza Serikali kwa uwekezaji huo mkubwa akisema mtambo huo utawanufaisha kwa kiasi kikubwa wanafunzi na wakufunzi katika mafunzo yao.
Dkt. Lupala amesema mtambo huo una uwezo wa kuchanganya dawa, vipimo na maji kwa usahihi, hali itakayowawezesha wakufunzi kutoa mafunzo kwa vitendo na kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa teknolojia ya kutibu mbao.
“Mtambo huu wa kutibu mbao utasaidia sana katika ufundishaji. Wakufunzi watakapokuwa darasani watafundisha kwa vitendo, na wanafunzi wanapomaliza masomo yao hawatakuwa wageni wa teknolojia hii,” alisema Dkt. Lupala.
Ameongeza kuwa mtambo huo ni wa kisasa na haukuwahi kupatikana katika Kanda ya Kaskazini, hivyo unatarajiwa kutoa huduma katika mikoa ya Tanga, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Dkt. Lupala alisema mtambo huo umenunuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 100, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya viwanda vya misitu.
Amefafanua kuwa awali mtambo wa kutibu mbao ulikuwa unapatikana Mafinga pekee, hali iliyokuwa changamoto kwa wanafunzi wa Kanda ya Kaskazini.
“Kupitia programu zetu hapa chuoni, asilimia 90 ya wahitimu wa FITI huajiriwa katika sekta ya viwanda vya misitu, hivyo uwepo wa mtambo huu utaongeza ufanisi na ushindani wao katika soko la ajira,” aliongeza.
Kwa upande wao, baadhi ya wakufunzi chuoni hapo akiwemo Gabriel Mushi, wameeleza kufurahishwa na ujio wa teknolojia hiyo mpya wakisema utaongeza morali na ubora wa ufundishaji.
“Sisi wakufunzi hufurahi sana pale tunapomfundisha mwanafunzi kwa vitendo na kuona anaelewa kile anachofundishwa,” alisema Mushi.







