LANG'ATA-MWANGA.
MIKOPO umiza imeendelea kuibuka kuwa janga kubwa kwa wakazi wa Kata ya Lang’ata, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, hali inayodaiwa kuchangia ongezeko la watoto wa mitaani baada ya wazazi wao kukimbia makazi wakikwepa kudaiwa, kudhalilishwa na kunyang’anywa mali.
Kero hiyo iliwasilishwa na wakazi wa kata hiyo akiwemo Zainabu Shaban, Nuru Mandela na Ibrahim Saidi mbele ya Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika Jimbo la Mwanga.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi, Zainabu Shaban alisema watoto wengi wamejikuta wakikosa haki zao za msingi ikiwemo elimu, malezi bora na ulinzi, hali inayotishia mustakabali wa maisha yao.
Alidai kuwa wazazi wengi, hususan wanawake na vijana, wameingia kwenye mikopo yenye riba kubwa kwa matumaini ya kuboresha maisha yao, lakini wanaposhindwa kurejesha hulazimika kukimbia makazi yao kwa kuogopa kudhalilishwa na kunyang’anywa mali, huku wakiwaacha watoto wao wakihangaika mitaani.
“Kero yetu ni mikopo umiza, itatuua. Hapa kwetu kuna mikopo inaitwa Gebikagandula, mikopo ya Black, ASA na Sukuma. Mikopo yote hii tunakopa lakini hali zetu ni mbaya sana,” alisema Zainabu.
Aliongeza kuwa wakazi wamekuwa wakiomba mikopo isiyo na riba inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri, lakini mchakato wake umejaa urasimu mkubwa.
Alisema baadhi ya wananchi hutumia hadi shilingi 100,000 kwa gharama za usajili na ufuatiliaji wa mikopo hiyo, lakini hawafanikiwi kuipata, hali inayowalazimu kukimbilia mikopo umiza.
Zainabu pia alidai kuwa baadhi ya vikundi hupewa mikopo zaidi ya mara tatu, wakati wakazi wa Lang’ata hawajawahi kunufaika hata mara moja.
“Leo tunamuomba Naibu Waziri atusaidie ili na sisi tuweze kupata mikopo hiyo ya Serikali,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Nuru Mandela, mkazi wa Kijiji cha Kagongo – Lang’ata, alisema mikopo ya halmashauri imejaa urasimu mkubwa na kudai kuwa licha ya kuwepo kwa vikundi vingi vilivyosajiliwa, wanapofuatilia wanakumbana na usumbufu mkubwa.
Alidai kuwa mara nyingi mikopo hiyo huwanufaisha wananchi wa maeneo mengine ya Mwanga, huku wakazi wa Lang’ata wakiachwa nyuma licha ya kutumia gharama kubwa za nauli na muda kufuatilia.
Mandela aliongeza kuwa wamekuwa wakiunda vikundi vya ujasiriamali kwa lengo la kupata mikopo isiyo na riba, lakini hukosa fursa hiyo kutokana na urasimu uliopo katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, hali inayowalazimu kukimbilia mikopo umiza.
Aidha, alisema changamoto nyingine kubwa ni kukosekana kwa vitambulisho vya Taifa (NIDA), akidai kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa Lang’ata hawana NIDA, hali inayowakosesha sifa ya kupata mikopo ya Serikali.
Diwani wa Kata ya Kileo, Kuria Msuya, alimuomba Naibu Waziri kuhakikisha mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya vikundi maalum unawafikia walengwa bila ubaguzi.
Akijibu kero hizo, Naibu Waziri Dkt. Ngwaru Maghembe alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha mikopo isiyo na riba inawafikia wananchi waliokusudiwa, hususan vijana, wanawake na makundi maalum kupitia halmashauri.
Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo hiyo, na aliahidi kufuatilia ili isitawaliwe na urasimu.
Kuhusu changamoto ya kukosekana kwa vitambulisho vya Taifa, Dkt. Ngwaru alisema ofisi yake imeichukua changamoto hiyo na hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa NIDA kwa wakati.





