VYUO VYA MISITU FITI, OLMOTONYI VYAJIPANGA KUBORESHA MITAALA YA ELIMU YA MISITU

 MOSHI-KILIMANJARO

UONGOZI wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI),  umesema umejipanga kuboresha mitaala ya elimu ya misitu ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya misitu nchini na kimataifa.

Mkuu wa chuo cha FITI Dk. Zakari Lupala aliyasema hayo jana, wakati wa kufungua warsha ya siku tano iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa FITI, ikilenga kupitia na kuboresha mitaala ya mafunzo ya misitu.

“Tupo kwenye warsha ya kupitia maboresho ya mitaala ya misitu ambayo tuliandaa kupitia mradi wa pamoja, lengo letu ni kuhakikisha mitaala yetu inatoa elimu inayoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira,” alisema Dk. Lupala.

Dk. Lupla alieleza kuwa mradi huo ni ushirikiano kati ya FITI, Chuo cha Misitu Olmotonyi, Chuo cha Misitu Zambia, taasisi za elimu kutoka Finland na Chuo cha LUO kutoka Estonia, chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).


“Mradi huu ni chombo muhimu kwa sisi viongozi wa vyuo na watunga mitaala ili kuhakikisha programu zetu zinawajengea wanafunzi ujuzi wa kushindana katika soko la ajira, wakiwemo waajiriwa serikalini na sekta binafsi,” alisema.

Dk. Lupala alisisitiza kuwa mitaala inayotumika katika vyuo vya elimu ya misitu inapaswa kurekebishwa mara kwa mara ili iendane na mabadiliko ya kimataifa na fursa mpya zinazojitokeza katika sekta ya misitu.

“Tunafahamu kuwa sera mpya ya elimu nchini Tanzania inalenga kujenga ujuzi zaidi kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya msingi. FITI imechukua hatua hiyo kwa kufanya mapitio ya mitaala kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi,” aliongeza.


Alisema serikali imetoa nafasi kubwa kwa vijana kupata elimu inayojikita katika ujuzi ili kuwasaidia kuingia kwenye ajira au kuanzisha biashara zao, hasa katika sekta ya misitu.

“Chuo chetu kitasimama imara kufanikisha mabadiliko haya ya kisera kwa kushirikiana na wadau wote katika sekta ya misitu na viwanda vya misitu nchini,” alisema Dk. Lupala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi l Dk. Joseph Makero, alisema warsha hiyo imewakutanisha wataalam kutoka Finland, Zambia, na Estonia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka mitatu unaolenga kuimarisha elimu ya misitu kwa kutoa mafunzo yenye ujuzi na ubunifu kwa usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu.

“Lengo ni kuwajengea uwezo wakufunzi wa misitu Tanzania na Zambia ili waweze kufundisha kwa kutumia teknolojia za kisasa na mbinu za kisayansi zinazotekelezeka kwa vitendo,” alisema Dk. Makero.

Mradi huo ulianza rasmi Januari 2025 hadi Desemba 2027 na unalenga maeneo matano muhimu, ikiwemo uboreshaji wa utawala wa vyuo, kuimarisha mahusiano na wadau wa sekta ya misitu, uundaji wa mitaala inayokidhi viwango vya kisasa, programu za kubadilishana wanafunzi na walimu kimataifa pamoja na ujenzi wa uwezo kwa wakufunzi na viongozi wa taasisi

Aliongeza kuwa “Baada ya kupata mafunzo, wataalamu wetu watawafundisha wanafunzi kwa vitendo badala ya nadharia pekee, hii itawawezesha kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa misitu,” alisisitiza Dk. Makero.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.