MOSHI-KILIMANJARO.
Mkazi wa mjimwema, Kata ya Miembeni katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, James Joseph Chombo (63), amemshukuru mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, kwa kugharamia matibabu ya mtoto wake anayesumbuliwa na ugonjwa wa figo kwa muda mrefu.
Akizungumza Oktoba 13, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari J.K. Nyerere, Chombo alisema msaada huo umetolewa katika kipindi kigumu ambapo familia imeelemewa na gharama kubwa za matibabu.
“Natoa shukrani za dhati kwa Ibrahim Shayo kwa moyo wake wa huruma na uzalendo alioonesha kwa familia yangu, alitusaidia kiasi cha shilingi milioni tatu (3,000,000), fedha ambazo zilitumika kwa ajili ya matibabu ya mtoto wangu Joseph ambaye amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo tangu mwaka 2017,” alisema Chombo.
Kwa mujibu wa Chombo, kijana wake Joseph anahitaji kusafishwa figo kila baada ya siku tatu kutokana na mirija ya figo kupata aleji, na kila zoezi la usafishaji hugharimu shilingi 150,000 kwa wiki mbili, hadi sasa, matibabu yamekuwa yakifanyika katika hospitali ya St. Joseph na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Hadi sasa bado tatizo halijajulikana linatokana na nini, madaktari wametushauri kwamba, kutokana na umri wake mdogo, njia pekee ya kumsaidia ni kumpandikiza figo mpya, ambapo gharama ya upasuaji huo inakadiriwa kuwa kati ya shilingi milioni 40 hadi 50,” aliongeza.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali na watu wenye mapenzi mema kujitokeza kumsaidia kifedha ili mtoto wake aweze kupata huduma ya upandikizaji figo, akisema kuwa familia yake haina uwezo wa kugharamia kiasi hicho kikubwa cha fedha.
“Naomba msaada wa fedha kwa yeyote atakayeguswa, gharama hii ni kubwa sana kwangu na familia yangu haiwezi kuimudu, kijana wangu anaendelea kuteseka,” alisema kwa uchungu.
Kwa mujibu wa tafiti za afya nchini, wagonjwa wa figo wanaendelea kuongezeka, huku wengi wakikabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za matibabu, hasa huduma ya usafishaji damu na upandikizaji figo.
KWA MAWASILIANO ZAIDI UNAWEZA KUWASILIANA NA BABA YAKE MZAZI JAMES JOSEPH CHOMBO KWA NAMBA HII; 0692-79 39 39.








