MOSHI-KILIMANJARO.
Changamoto sugu ya mfumo wa maji taka katika Mtaa wa Relini, Kata ya Bomambuzi, imekuwa kilio kikuu katika kampeni za mgombea udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Juma Raibu, ambaye amewaomba wananchi kumpa ridhaa ili aweze kushinikiza suluhisho ndani ya Baraza la Halmashauri.
Akihutubia mamia ya wakazi wa kata hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana, Raibu alisema hali ya miundombinu ya maji taka katika mtaa huo ni mbaya kiasi cha kuhatarisha afya za wakazi na kutishia mazingira ya mji wa Moshi.
“Changamoto ya maji taka ni kubwa, kama haitashughulikiwa haraka, inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa mkinitunuku kura Oktoba 29, nitaenda kupigania suluhisho lake kupitia mamlaka husika,” alisema Raibu kwa msisitizo.
Pamoja na hilo, alitaja matatizo mengine yanayoikabili kata hiyo kuwa ni pamoja na barabara ya M-Pesa ambayo ipo katika hali mbaya na imekuwa kikwazo kwa wananchi kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
“Barabara hii haipitiki vipindi vingi vya mwaka, nitahakikisha Tarura wanaitengeneza ili wananchi wasiendelee kuteseka,” aliongeza.
Kuhusu masuala ya ardhi, Raibu alisema kuna migogoro mingi inayotokana na ukosefu wa hati, na kwamba akipewa nafasi atahakikisha wataalamu wa ardhi wanapita kufanya upimaji na kuwapatia wananchi hati miliki.
Katika mkutano huo, Raibu pia alitumia nafasi hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za maendeleo katika Kata ya Bomambuzi ndani ya kipindi cha miaka minne tu.
“Kupitia uongozi wa Rais Samia, tulipokea Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya, kabla ya hapo, akinamama wajawazito walikosa huduma muhimu, lakini sasa wanahudumiwa vizuri,” alieleza.
Aliongeza kuwa serikali pia imetoa Sh milioni 576 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Bomambuzi, ambayo tayari imeanza kufanya kazi, na Sh milioni 386 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Mshikamano.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, Raibu alisema serikali imetoa Sh milioni 800 kwa ajili ya uboreshaji wa barabara ndani ya kata hiyo.
“Naomba tena kura zenu ili niweze kuingia kwenye Baraza la Madiwani na kuendelea kupigania changamoto hizi zitatuliwe kikamilifu,” alihitimisha.
Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa na mitaa unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2026, ambapo wananchi watachagua madiwani na viongozi wa maeneo yao.


























