VIONGOZI WA DINI WAENDELEA KUMMIMINIA BARAKA MGOMBEA UBUNGE MOSHI MJINI

MOSHI-KILIMANJAO.

Baadhi ya viongozi wa dini kutoka maeneo mbalimbali ya Moshi Mjini wameendelea kutoa baraka na dua kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, wakisema kuwa wameona wazi mkono wa Mungu ukimwongoza katika safari yake ya kisiasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara na ibada, viongozi hao wamesema kuwa mgombea huyo amekuwa akionesha moyo wa huruma, upendo na kuguswa na mahitaji ya watu, bila kujali tofauti za imani au itikadi.

"Tumeshuhudia akienda makanisani, misikitini, na kwenye taasisi mbalimbali za kiroho na kijamii akitoa misaada na kuchangia mali zake, alizobarikiwa na Mwenyezi Mungu, hii ni ishara ya mtu aliyejitoa kwa ajili ya watu wake," alisema mmoja wa viongozi wa dini waliokuwepo katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Oktoba 22, 2025 katika mtaa Kigongoni kata ya Shirimatunda.

Kiongozi huyo wa kiroho, ameongeza kuwa matendo hayo ya ukarimu na kujitoa kwake katika jamii, yamekuwa sehemu ya maombi yao ya muda mrefu, na sasa wanayaona yakitimia kupitia uteuzi wake wa kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi ujao.

"Tumeona akigusa maisha ya watu wenye uhitaji na hata wasio na uhitaji, ameonesha kuwa ni kiongozi anayeguswa na matatizo ya watu wake, tunaamini Mungu amemwongoza hadi hatua hii ya kugombea,” alisema kiongozi huyo wa dini.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, hatua ya kumpa baraka mgombea huyo wa ubunge jimbo la Moshi mjini ni sehemu ya wajibu wao wa kiroho katika kuwaombea wale wanaotafuta uongozi ili wahudumu kwa haki, busara na kwa kumcha Mungu.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.