MGOMBEA UBUNGE MOSHI MJINI AHAIDI KUPIGANIA WAZEE WALIOSAHAULIWA NA TASAF

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini amesema kuwa kazi yake ya kwanza endapo atachaguliwa itakuwa ni kupigania wazee ambao hawajanufaika na mpango wa TASAF, ili nao waweze kunufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini.

Akizungumza Oktoba 24,2025 katika mkutano uliofanyika eneo la Liwali Street, Kata ya Bondeni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mgombea huyo alisema kuwa wazee wengi wenye sifa za kupata fedha za mpango huo wameachwa nyuma bila sababu za msingi.

Alisema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni, atahakikisha anasimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ili wazee wote wanaostahili waweze kuingizwa kwenye orodha ya walengwa.

Aidha, alibainisha kuwa licha ya serikali kuendelea kutoa fedha kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini, bado wapo wananchi wanaostahili lakini hawajawahi kunufaika na msaada huo.

Kuhusu changamoto ya mfumo wa maji taka katika Manispaa ya Moshi, mgombea huyo alionyesha kusikitishwa na hali ya maji taka kuendelea kutiririka mitaani.

Alisema, endapo wananchi watamchagua, atahakikisha mfumo huo unaboresha kwa kujengwa upya ili kulinda afya za wakazi wa Moshi.

Akizungumzia suala la viwanda, alisema awali Moshi ilikuwa na viwanda vingi vilivyotoa ajira kwa vijana, lakini kwa sasa karibu vyote vimekufa.

Aliahidi kupigania kufufuliwa kwa viwanda au kuanzishwa kwa angalau kiwanda kimoja cha kutengeneza juisi, kutokana na wingi wa matunda yanayozalishwa katika mkoa wa Kilimanjaro na Tanga.

Kuhusu Soko la Manyema, mgombea huyo aliwaomba wananchi kumpa kura ili aweze kulitetea bungeni, kwa lengo la kuhakikisha soko hilo linapata hati halali ya umiliki na kujengwa upya, ili wafanyabiashara waweze kufanya kazi katika mazingira bora zaidi.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.