MGOMBEA UDIWANI BONDENI AHAIDI KUWAWEZESHA VIJANA KUPATA UJUZI KUPITIA VETA

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea udiwani wa Kata ya Bondeni, Alhaji Hajji Fundi, amesema katika kipindi hiki cha Sayansi na Teknolojia, vijana wanahitajika zaidi kwenye soko la ajira la sasa, ambalo linahitaji watu wenye ujuzi na ubunifu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Mtaa wa Liwali Kata ya Bondeni, mgombea huyo alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa diwani, atahakikisha kila mwaka vijana 10 hadi 20 kutoka kata hiyo wanapelekwa katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kupunguza utegemezi wa ajira za serikali.

"Leo hii hakuna fundi seremala, fundi ujenzi, fundi rangi au fundi wa kuchomelea anayehitajika kuwa na shahada ili aweze kupata ajira, kinachohitajika ni ujuzi na ubunifu, nitahakikisha vijana wa Bondeni wanapata nafasi hizo kupitia VETA,” alisema Alhaji Fundi.

Aliongeza kuwa, endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa diwani, atagharamia ada za vijana hao wanaopelekwa VETA ili waweze kupata ujuzi na hatimaye kufungua viwanda vidogo vitakavyotoa ajira kwao na wenzao.

Kuhusu utawala bora, Alhaji Fundi, alisema kuwa Kata ya Bondeni inakabiliwa na changamoto za miundombinu ya utawala bora, ikiwemo kukosa ofisi za Serikali za Mitaa.

"Ninaahidi mbele yenu kuwa nikichaguliwa kuwa diwani, nitajenga ofisi za Serikali za Mitaa katika mitaa yote miwili ya kata hii,” alisema.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa ofisi maalumu za kushughulikia masuala ya ndoa, mirathi pamoja na migogoro mingine ya kifamilia, ambapo kwa sasa wananchi hulazimika kwenda kwenye baraza la usuluhishi la wazee.

“Ndani ya miaka miwili yq uongozi wangu, baada ya kuchaguliwa, nitahakikisha tunapata ofisi ya usuluhishi ndani ya Kata yetu ya Bondeni,” aliahidi.

Kuhusu Soko la Manyema, mgombea huyo alisema atalisimamia na kulitetea soko hilo ili wafanyabiashara na wajasiriamali waendelee kufanya biashara zao katika eneo hilo.

“Soko la Manyema limekuwepo kwa zaidi ya miaka 10. Wafanyabiashara wamewekeza muda na nguvu zao hapo, hivyo sitakubali waondolewe, wataendelea kubaki katika soko hilo,” alisema.

Aidha, Alhaji Fundi, aliahidi kushughulikia changamoto ya Zahanati ya Bondeni kwa kuhakikisha inapandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya kitakachotoa huduma bora zaidi kwa wakazi wa kata hiyo.

"Nimeamua kuchukua hatua ya kuhakikisha zahanati yetu inapanuliwa na kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya ili wananchi wapate huduma za uhakika,” alisema Fundi.


















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.